DRC-EBOLA-AFYA

Idadi ya vifo kufuatia mlipuko wa Ebola yafikia 201 mashariki mwa DRC

Kituo kinachotoa huduma kwa wagonjwa wa Ebola (CTE) Mangina, Kivu Kaskazini, DRC.
Kituo kinachotoa huduma kwa wagonjwa wa Ebola (CTE) Mangina, Kivu Kaskazini, DRC. Florence Morice/RFI

Tangu mwanzo wa ugonjwa hatari wa Ebola kuripotiwa kwenye majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri mashariki mwa DRC, Wizara ya Afya, nchini humo imesema kesi 329 zimeripotiwa, ikiwa ni pamoja na vifo 201.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa wizara hiyo, takwimu hii ni kubwa kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka wa 1976 mjini Yambuku, katika mkoa wa Equateur, ambako kwa mara ya kwanza ugonjwa huo ulizuka nchini DRC.

Waziri wa Afya anasema DRC haijawahi kukumbwa na ugonjwa hatari kama huu ulioko sasa.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari wizara ya afya imesema tangu kuzuka kwa ugonjwa huo idadi ya waliokufa kutokana na Ebola mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imeongezeka na kufikia watu 200 huko Beni.

Ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na shirika la Afya duniani WHO, inasema makundi ya waasi yamekuwa yakiwashambulia wauguzi, kuwapiga na baadhi kuuliwa huku raia wa kawaida wakitishwa.

Juma lililopita, maafisa watatu wanaotoa kinga dhidi ya Ebola walizuiliwa na wanamgambo wa Mai-Mai katika kijiji cha Matembo, kati ya Beni na Butembo huko Kivu kaskazini.

Kuzorota kwa usalama pamoja na ongezeko la idadi ya watu ni miongoni mwa changamoto zilizoko katika kupambana na ugonjwa huo hatari miaka kadhaa iliyopita.

Tume ya Umoja wa Mataifa Monusco imesema imepanga mikakati ya kuwalinda waunguzi wanaotoa chanjo dhidi ya Ugonjwa huo.