LIBYA-MAZUNGUMZO-SIASA-USALAMA

Mkutano wa Libya wagubikwa na sintofahamu

Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte (kushoto) na Marshal Khalifa Haftar, anayedhibiti mashariki mwa Libya, Novemba 12, 2018 Palermo (Italia)
Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte (kushoto) na Marshal Khalifa Haftar, anayedhibiti mashariki mwa Libya, Novemba 12, 2018 Palermo (Italia) © AFP

Mkutano wa kutafutia suluhu mgogoro wa Libya, ulioanza siku ya Jumatatu usiku katika mji wa Palermo huko Sicily, nchini Italia unaendelea leo Jumanne. Wadadisi wanasema itakuwa vigumu kuwakutanisha wadau wote katika mgogoro unaoikabili libya tangu kuuawa kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Muammar Gaddafi.

Matangazo ya kibiashara

Marshal Khalifa Haftar, ambaye majeshi yake yanadhibiti mashariki mwa Libya, ameendelea na msimamo wake wa kutoshiriki katika mazungumzo hayo, baada ya kususia siku ya Jumatatu usiku chakula cha jioni kilichoandaliwa na kiongozi wa Italia Giuseppe Conte.

Alipofika jioni, alipokelewa na Bw Conte lakini dakika chache baadae alichukua hatua ya kuondoka eneo kuliko kuwa kukifanyika mkutano huo. "Mchango wako kwa mkutano ni muhimu," Conte alimwambia marshal Khalifa Haftar kabla ya yeye kuondoka.

Marshal Haftar anapinga kuketi kwenye meza moja na baadhi ya washiriki katika mkutano huo, ambao anawachukulia kama wanamgambo wa Kiislamu wenye itikadi kali, kwa mujibu wa washirika wake wa karibu.

Miaka saba imepita baada ya rais wa Libya Muammar Gaddafi kuuawa Oktoba 20 mwaka 2011 mjini Syrte na wapiganaji waliojinasibu kupigania mabadiliko.

Miaka saba baadae makundi kadhaa yameoneoneka kukita mizizi yake nchini humo na kuendesha mapigano huku raia wakitaabika na kujuta.

Raia wengi nchini Libya wanasifu utawala wa Gaddafi, wakisema “wakati wa utawala wa Gaddafi hali ilikuwa nzuri isiokuwa na mfano licha ya matatizo madogo kuweza kujitokeza”.

Kutokana na hali inavyozidi kuwa mbaya, raia wa Libya wanaonekana wakiwa na kumbukumbu nzuri za utawala wa Gaddafi.

Makundi yanayojinasibu kupigana vita vitakatifu yanaendesha mauaji kila kukicha na kushindwa kuafikiana katika michakato ya amani.