CONGO-UN-MOKOKO-HAKI

Umoja wa Mataifa: Jenerali Mokoko azuiliwa kinyume cha sheria Congo-Brazzaville

Aliyekuwa mgombe urais, Jenerali mstaafu Jean-Marie Michel Mokoko, wakati wa kesi yake ikianza kusikilizwaa, Mei 7, 2018.
Aliyekuwa mgombe urais, Jenerali mstaafu Jean-Marie Michel Mokoko, wakati wa kesi yake ikianza kusikilizwaa, Mei 7, 2018. RFI / Florence Morice

Umoja wa Mataifa umeishtumu Congo-Brazzaville kwa kumzuia kinyume cha sheria Jean-Marie Michel Mokoko. Mokoko, mgombea wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2016, alihukumiwa mwezi Mei mwaka huu hadi miaka 20 jela kwa madai ya kuhujumu usalama wa taifa na kumiliki silaha za kivita na vifaa vya jeshi kinyume cha sheria.

Matangazo ya kibiashara

Wanasheria wake walikataa rufaa kwa kupinga uamuzi huo. Wanasema wanasubiri tarehe iliyopangwa ili waweze kuonyesha udhalimu unaofanyiwa mteja wao. Lakini pia wanasheria wa Mokoko waliwasilisha malalamiko yao mbele ya tume ya Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuiliwa kinyume cha sheria kwa Jenerali Jean-Marie Mokoko. Tume ya Umoja wa Mataifa tayari imebaini kwamba Jenerali Mokoko anazuiliwa kinyume cha sheria.

Tume hiyo ya Umoja wa Mataifa, hata hivyo, imeomba Jenerali Jean-Marie Michel Mokoko aachiliwe huru mara moja bila masharti.

Jenerali mstaafu Mokoko, aliyekuwa mgombea wa urais wa chama cha upinzani cha FROCAD, alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela, baada ya kupatikana na hatia ya kuhujumu usalama wa taifa na kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Waendesha mashtaka katika kesi hiyo wamesema Mokoko na watuhumiwa wenzake kadhaa wamepatikana na hatia ya kukusanya silaha kinyume cha sheria mwaka 2005, kwa lengo la kuipindua serikali.

Mokoko ambaye aligombea urais katika uchaguzi uliofanyika mapema mwaka 2016, alitiwa nguvuni na vyombo vya usalama mwezi Juni mwaka huo.

Serikali ya Rais Denis Sassou Nguesso imekuwa ikimtuhumu jenerali huyo mstaafu ambaye alikuwa mpatanishi katika mchakato wa mgawanyo wa madaraka wakati wa vita vya ndani vilivyotokea nchini humo katika muongo wa 1990, kuhusika na jaribio la mapinduzi ya kijeshi la mwaka 2007.

Mokoko alitunukiwa tuzo ya heshima ya Commander of the Congolese Order of Merit na kwa msingi huo wakili wake Philippe Esseau, anasema hakupaswa kukamatwa, kushtakiwa wala kuhukumiwa.