MADAGASCAR-UCHAGUZ

Uchaguzi: Marais 2 wa zamani wa Madagascar kuchuana kwenye duru ya pili mwezi Desemba

Raia wa Madagascar akipiga kura katika uchaguzi wa hivi karibuni.
Raia wa Madagascar akipiga kura katika uchaguzi wa hivi karibuni. ALEXANDER JOE / AFP

Viongozi wawili wa zamani wa Madagascar, Andry Rajoelina na Marc Ravalomanana, wameibuka vinara katika uchaguzi mkuu wa hivi karibuni, wakati huu matokeo ya hapo jana yakionesha kuwa marais hawa watachuana katika duru ya pili mwezi ujao.

Matangazo ya kibiashara

Kwa matokeo yaliyopo hadi sasa hakuna mgombea kati ya hawa wawili aliyefikisha zaidi ya asilimia 50 inayotakiwa kwa mgombea kupata ili kuibuka mshindi katika raundi ya kwanza.

Matokeo yaliyotolewa na tume ya uchaguzi nchini humo CENI, yanaonesha kuwa Rajoelina amepata asilimia 39.19 ya kura na Ravalomanana amepata asilimia 35.29 ya kura.

Uchaguzi wa duru ya pili umepangwa kufanyika Desemba 19.

Rais Hery Rajaonarimampianina ambaye alikuwa anawania kuteuliwa kwa mara nyingine kuendelea kuongoza taifa hilo, alipata asilimia 8,84 ya kura, imesema taarifa ya tume ya uchaguzi ambayo imeongeza kuwa asilimia 54.3 ya watu walijitokeza kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Wagombea wote watatu kati ya 36 wamelalama kuhusu uwepo wa udanganyifu uliofanywa na tume ya uchaguzi na kwamba huenda kukashuhudiwa wagombea wengi wakikimbilia mahakamani kuyapinga.

Rais wa tume ya uchaguzi CENI, Hery Rakotomanana amesema tume yake ilitumia vigezo vitatu kuandaa uchaguzi wa mwaka huu ambavyo ni, uwazi, huru na haki.

Wagombea wote wawili walioibuka vinara wameapa kwenda mahakamani kila mmoja akieleza matumaini kuwa atatangazwa mshindi na mahakama.

Nchi ya Madagascar ni moja ya mataifa masikini duniani kwa mujibu wa wa takwimu za benki ya dunia, ambapo watu wanne kati ya watano wanaishi chini ya dola moja.

Waangalizi wa umoja wa Ulaya walisema Jumatatu ya wiki hii kuwa wagombea karibu wote walikiuka sheria za uchaguzi kabla ya uchaguzi wa November 7 lakini wakahitimisha kuwa uchaguzi ulifanyika katika mazingira ya uwazi na haki.

Ravalomanana na mwenzake Rajoelina wote walizuiliwa kugombea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2013 baada ya shinikizo la kimataifa ili kuepusha kujirudia kwa vurugu zilizoshuhudiwa mwaka 2009.

Ravalomanana na Rajoelina ni maadui wa kisiasa na hii ni mara ya kwanza kwa viongozi hawa kushinda kupitia njia ya upigaji kura.

Ravalomanana aliongoza taifa hilo kati ya mwaka 2002 hadi 2009 alipopinduliwa na jeshi ambalo lilimuweka madarakani Rajoelina aliyetawala hadi mwaka 2014.

Jaribio la mwanzoni mwa mwaka huu la rais Rajaonarimampianina kutaka kurekebisha sheria za uchaguzi lilishindakana baada ya kutokea maandamano makubwa ya kupinga hatua yake.

Waangalizi wa umoja wa Afrika wametoa wito kwa wagombea wote kujiepusha na utoaji wa matamshi ambayo huenda yakasababisha vurugu ambapo pia umewataka waheshimu utawala wa sheria.