COTE D'IVOIRE-ICC-HAKI

Kesi ya Gbagbo/Blé Goudé ICC: Wanasheria wa Charles Blé Goudé kusikilizwa

Charles Blé Goudé mbele ya majaji wa ICC, Januari 28, 2016.
Charles Blé Goudé mbele ya majaji wa ICC, Januari 28, 2016. © Peter Dejong / POOL / AFP

Kesi ya rais wa zamani wa Cote d'Ivoire Laurent Gbagbo na mtuhumiwa mwenzake Charles Blé Goudé inatarajiwa kusikilizwa tena leo Jumatatu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mjini Hague. Wanasiasa hawa wawili wanatuhumiwa uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa kuhusika katika machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2010-2011.

Matangazo ya kibiashara

Leo Jumatatu, wanasheria wa Charles Blé Goudé watakuwa nafasi ya kutetea mteja wao. Lengo lao ni kuonyesha kwamba mteja wao ni "mtu wa amani". Mwendesha mashtaka wa ICC anamshtumu kiongozi wa zamani wa vuguvugu la vijana wa chama tawala wakati huo (Cojep), kwamba aliwatolea wito vijana hao kujihusisha na vitendo vya ukatili dhidi yawafuasi wa Alassane Ouattara wakati wa mgogoro wa baada ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa mwandishi wa RFI katika mji wa Hague, Bineta Diagne, Mwendesha mashtaka wa ICC anamuelezea Charles Blé Goudé kama "kiongozi wa wanamgambo wanaounga mkono Gbagbo." kiongozi wa zamani wa vuguvugu la vijana wa chama tawala wakati huo nchini Cote d'Ivoire (Cojep) anakabiliwa na mashitaka kama yale yanayomkabili Laurent Gbagbo, kwa kuhusika kwa matukio makubwa 5 baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2010, " amesema Mwendesha Mashitaka wa ICC.

"Kwa matukio hayo, kunajiongeza matukio mengine 20 yaliyotokea katika mji wa Abidjan kati ya mwaka 2010 na 2011. Miongoni mwa matukio hayo, kuna makabiliano yaliyotokea wakati wa maandamano karibu na makao makuu ya Shirika la Utangazaji la RTI Desemba 16, 2010, ukandamizaji dhidi ya maandamano ya wanawake waliokuwa wakiunga mkono Alassane Ouattara tarehe 3 Machi 2011 na mfululizo wa machafuko katika kata jirani ya Yopougon Aprili 12, 2011," ameongeza.

Mwendesha mashtaka anamtuhumu Charles Ble Goude kwamba alitoa hotuba inayochochea chuki, ambayo ilizusha mchafuko katika kipindi hicho cha mgogoro. Upande wa mashtaka unaamini kwamba kiongozi huyo wa kisiasa alihusika katika vifo vya mamia ya watu nchini Cote d'Ivoire.

Charles Blé Goudé ambaye anazuiliwa jela tangu mwezi Machi 2014 katika gereza la Scheveningen, karibu na ICC, amekanusha madai hayo na kusema kuwa yeye si "mwanamgambo". Wanasheria wake wanamuelezea kuwa ni "mtu wa amani", "tu mwenye upendo", ambaye anafahamika kwa jina maarufu la "Kigogo wa mitaani".