DRC-AFYA-EBOLA

Mapambano dhidi ya Ebola yaanza tena mashariki mwa DRC

Kituo kinachotoa huduma kwa wagonjwa wa Ebola (CTE) Mangina, Kivu Kaskazini, DRC.
Kituo kinachotoa huduma kwa wagonjwa wa Ebola (CTE) Mangina, Kivu Kaskazini, DRC. Florence Morice/RFI

Mapambano dhidi ya mlipuko wa Ebola katika wilaya ya Beni mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yameanza tena baada ya kusitishwa kwa muda mfupi kutokana na mapigano kati ya waasi na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, (MONUSCO), Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza.

Matangazo ya kibiashara

"Siku ya Jumapili, shughuli zote zilizinduliwa tena, ikiwa ni pamoja na chanjo," imesema WHO katika taarifa hiyo.

Siku ya Jumamosi, Wizara ya Afya ya DRC ilisema kuwa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola katika eneo la Beni yalisitishwa baada ya mapigano kati ya waasi na majeshi, "mita chache kutoka eneo ambalo watu walioambukizwa Ebola wanakopewa matibabu, lakini pia karibu na hoteli za watalaam wa afya na kuzua wasiwasi".

Siku ya Ijumaa usiku, walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo (MONUSCO) walizima mashambulizi mapya ya kundi la waasi wa ADF "baada ya masaa kadhaa ya mapigano" katika wilaya Boikene, kaskazini mwa Beni, Wizara ya Afya ya DRC imesema.

Kundi la waasi wa Uganda la Allied Democratic Forces (ADF), ambalo liliua mamia ya raia tangu 2014 na kuuawa Walinda amani wasiopungua saba katika mapigano ya wiki hii iliyopita, lilitaka "kuendesha shambulizi dhidi ya moja ya kambi za MONUSCO", kwa mujibu wa taarifa rasmi ya serikali ya DRC.

Siku ya Jumapili, raia wawili waliuawa katika shambulio la ADF huko Mukoko, kilomita 36 kaskazini mwa Beni, chanzo cha shirika la kiraia kimesema.

Shirika la afya duniani WHO limesema kuwa, wafanyikazi wake 16 walifanikiwa kuokolewa mjini Beni, baada ya kilipuzi kulenga nyumba waliyokuwa wanaishi.

Watalaam wanaonya kuwa iwapo hali hii itaendelea, maambukizi yataendelea kushuhudiwa na idadi ya vifo itaongezeka. Tangu mwezi Agosti, watu 213 wamepoteza maisha.