DRC-ELIMU-USALAMA

Chuo kikuu cha Kinshasa chaendelea kukumbwa na sintofahamu

Chuo Kikuu cha Kinshasa (UNIKIN) Januari 19, 2015.
Chuo Kikuu cha Kinshasa (UNIKIN) Januari 19, 2015. © AFP

Hali ya sintofahamu yaendelea kujitokeza katika Chuko Kikuu cha Kinshasa (UNIKIN) nchini DRC. Hali hiyo ilianza Jumatatu Novemba 12 baada ya makabiliano kati ya wanafunzi na vikosi vya usalama. Wakati huo wanafunzi wawili walifariki dunia kutokana na majeraha ya risasi.

Matangazo ya kibiashara

Licha ya wito wa utulivu, na kumfungulia mashtaka mmoja wa maafisa wa polisi waliohusika na vifo vya wanafunzi hao, hali ya sintofahamu ilijitokeza kwa mara nyingine Jumatatu hii, Novemba 19. Walimu, wanafunzi na serikali wanatarajia Jumanne wiki hii kufanya mazungumzo ili kupatia ufumbuzi hali hiyo.

Kwa mujibu wa polisi mjini Kinshasa, sintofahamu iliyojitokeza Jumatatu wiki hii katika Chuo Kikuu cha Kinshasa (UNIKIN) ilisababishwa na kundi la wahuni walioingia katika Chuo Kikuu hicho.

Hali hiyo inatokea zikiwa zimesalia siku tatu kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi siku ya Alhamisi kuelekea Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Desemba 23.

"Wahuni kutoka Mbanza-Lemba (Kata masikini na yenye wakazi wengi iliyo karibu na Chuo Kikuu cha UNIKIN) ndio chanzo cha machafuko yaliyoripotiwa katika Chuo Kikuu cha Kinshasa ambapo hali ya utulivu imerejea. Polisi imerejesha usalama", Jenerali Sylvano Kasongo, mkuu wa polisi katika mji wa Kinshasa ameliambia shirika la Habari la AFP.

"Tuliwaachilia huru wanafunzi wote waliokamatwa, lakini wahuni bado wanashikiliwa na watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria," afisa huyo ameongeza.

"Makabiliano bado yanaendelea ... Polisi wanafyatua risasi hewani, na wanarusha gesi za machozi kwenye nyumba zetu. Tunajibu kwa kurusha mawe kwa kukabiliana na hali hiyo," alisema mwanafunzi katika Kitivo cha biolojia akiohojiwa Jumatatu mchana.na AFP.

"Polisi wako kila mahali kwenye Chuo hiki, wanakamata kila mpita njia, wanawaibia simu zao, fedha na mikoba yao. Tumeamua kurudi nyumbani," aliongeza mwanafunzi mwingine kutoka Kitivo cha Sayansi.

Wanafunzi wawili walifariki wiki iliyopita baada ya kupigwa risasi na polisi kwenye Chuo Kikuu cha Kinshasa (UNIKIN) wakati wakiandamana wakitaka visomo kuanza, baada ya mgomo wa waalimu.

"Afisa wa polisi aliyefyatua risasi alikamatwa, atahukumiwa kwa mujibu wa sheria," ameahidi Waziri wa Elimu ya Juu Steve Mbikayi.

Upinzani kupitia mgombea wao Martin Fayulu, umeshtumu "matumizi ya kupita kiasi ya vikosi vya usalama kwa kuzima maandamano ya wanafunzi" na "uhaba wa vifaa vya usalama nchini DRC".

Tangu Novemba 12, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha UNIKIN wanaandamana wakiomba mgomo wa walimu wao usitishwe. Mgomo ambao ulianza miezi miwili iliyopita jkuhusu masuala ya mishahara.

Mkutano wa waalimu wa Chuo Kikuu cha UNIKIN umepangwa kufanyika Jumatano wiki hii kuamua iwapo wataendelea na mgomo au la baada ya mazungumzo na serikali, kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini DRC.