DRC-SIASA

Upinzani waruhusiwa kusherehekea kurudi kwa mgombea wake Fayulu nchini DRC

Wafuasi wa mgombea wa urais DRC Martin Fayulu wakiingia mitaani baada ya muungano wa upinzani kumteua kama mgombea, Kinshasa, DRC, Novemba 12, 2018.
Wafuasi wa mgombea wa urais DRC Martin Fayulu wakiingia mitaani baada ya muungano wa upinzani kumteua kama mgombea, Kinshasa, DRC, Novemba 12, 2018. © REUTERS

Serikali nchini DRC imeruhusu upinzani nchini humo kuandamana Jumatano wiki hii mjini Kinshasa kwa kumpokea mmoja wa wagombea wake katika uchaguzi wa urais, Martin Fayulu, ambaye anarejea leo.

Matangazo ya kibiashara

Fayulu anarejea nchini siku moja kabla ya kuanzishwa kwa kampeni ya uchaguzi wa desemba 23, ambapo siku ya alhamisi Tume Huru ya Uchaguzi (CENI) imejipanga kuzindua kuanzishwa kwa kampeni hizo.

Gavana wa mji wa Kinshasa amewataka wafuasi wa Fayulu "kuwasiliana" na mkuu wa polisi katika mji wa Kinshasa "kwa amaelekezo zaidi".

Fayulu anatarajia kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ndjili mjini Kinshasa Jumatano mchana akitokea Ulaya kwa ndege ya kawaida.

Hayo yanajiri wakati mapema wiki hii mgombea wa muungano wa vyama vinavyoshiriki serikalini nchini DRC (FCC) Emmanuel Ramazani Shadary alinadi mpango wake, iwapo atafanikiwa kuchaguliwa kama rais wa nchi hiyo. Itahitaji dola bilioni 86 ili kutekeleza mpamgo huo kwa muda wa miaka mitano. Pia aliahidi kuimarisha mamlaka ya nchi.

Wanasiasa wawili wa upinzani: Felix Tshisekedi wa UDPS na Vital Kamerhe wa UNC waliondoa saini zao wakionyesha kutomuunga mkono Martin Fayulu, kama mgombea mmoja atayewakilisha upinzani wa DRC katika Uchaguzi Mkuu wa Desemba 23.

Siku ya Jumatatu Kanisa Katoliki nchini DRC liliitaka serikali ya nchini hiyo "kuhakikisha na kutoa nafasi kwa uhuru wa kuandamana kwa wagombea wote" nchini DRC ambapo maandamano ya upinzani mara nyingi huwa yakipigwa marufuku au kusambaratishwa na polisi.