DRC-UCHAGUZI-SIASA

Kampeni za uchaguzi zaanza, hali ya wasiwasi yatanda DRC

Mashine ya kupigia itakayotumiwa katika uchaguzi wa Desemba 23 nchini DRC, Februari 21, 2018.
Mashine ya kupigia itakayotumiwa katika uchaguzi wa Desemba 23 nchini DRC, Februari 21, 2018. John WESSELS / AFP

Kampeni za uchaguzi mkuu Wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimeanza hii leo siku ya Alhamisi ikiwa ni hatua ya mwisho ya kuelekea uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Desemba 23.

Matangazo ya kibiashara

Kampeni hizi zimeanza leo wakati wanasiasa wa nchi hiyo wanaoishi nje na walioruhusiwa kushiriki katika uchaguzi huo wakiwa wameanza kurejea nyumbani kwa ajili ya kampeni za uchaguzi huo, miongoni mwao Martin Fayulu Madidi ambaye aliteuliwa hivi karibuni na wapinzani katika mkutano wa Geneva, kupeperusha bendera ya Upinzani, ambapo wanasiasa wawili mashuhuri Felix Tshisekedi wa UDPS na Vital Kamerhe wa UNC waliondoa saini zao.

Kinyanganyiro kigumu kinachotarajiwa kushudiwa nchini humo ni kati ya Mgombea wa Upinzani Martin Fayulu na Mgombea mteule wa rais Joseph Kabila, ambaye anapeperusha bendera ya muungano wa vyama tawala FCC, Emmanuel Ramazani Shadary.

Wanasiasa nchini DRC wanatofautiana kuhusu matumizi ya mashine za kupigia kura ambapo tume inayosimamia uchaguzi inakabiliwa na changamoto ya kuwahamasisha wananchi kuhusu uchaguzi kupitia mfumo wa elekroniki.

Raia wengi nchini DRC hasa kwenye maeneo ya vijijni hawajawahi kutumia kompyuta, nchi hiyo ikiwa imekabiliwa na changamoto kadhaa, zikiwemo miundombinu mibovu, barabara mbovu, ukosefu wa usalama na uhaba wa umeme kila sehemu.

Kampeni hizi zinaanza leo Alhamii, inatarajiwa zitamalizika baada ya siku thelathini, kabla ya uchaguzi wa Desemba 23 mwaka huu.