DRC-UCHAGUZI-CENI-PPRD-SHADARY-KAMPENI

Kampeni za kisiasa zapamba moto nchini DRC

Rais wa DRC Joseph Kabila, wakati wa uzinduzi wa kampeni nchini DRC Novemba 22 2018
Rais wa DRC Joseph Kabila, wakati wa uzinduzi wa kampeni nchini DRC Novemba 22 2018 RFI

Kampeni za kisiasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, zinaendelea baada ya kuanza rasmi hapo jana, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa tarehe 23 mwezi Desemba.

Matangazo ya kibiashara

Ni kampeni zinazoendelea wakati huu, kukiwa na mvutano mkubwa kuhusu suala la matumizi ya mashine za kupigia kura, pamoja na changamoto za kiusalama, mashariki mwa nchi hiyo.

Chini ya mwezi mmoja, kuelekea kwenye Uchaguzi huu, kuna baadhi ya wanasiasa ambao wanaona kuwa hautafanyika.

“ Sehemu kubwa ya wagombea hawana uhakika kwamba uchaguzi utafanyika desemba 23 ya mwaka huu hiyo ni moja, pili..Kuna tatizo la watu kuwa na uwezo, kwa sababu ili kupiga kampeni nchini DRC inabidi mtu awe na uwezo mkubwa na unaotosha; na wengi wa wagombea wanakumbwa na ukosefu wa pesa,”

“Ukichukulia kudorora kwa uchumi wa nchi kwa muda wa miaka mingi, wengi wanaogopa kutumia pesa kubwa katika mazingira ambayo hawana uhakika kwamba kutakuwa uchaguzi wanahofia kwamba hawatafaidika na kitu.” amesema Bob Kabamba mtaalamu wa siasa za DRC na mtafiti wa masuala ya kisiasa katika Chuo Kikuu cha Liege nchini Ublegiji.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini DRC , Corneille Nangaa akizungumza na wanahabari jijini Kinshasa hivi karibuni
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini DRC , Corneille Nangaa akizungumza na wanahabari jijini Kinshasa hivi karibuni © JOHN WESSELS / AFP

Hata hivyo, Tume huru ya uchaguzi CENI inasema, uchaguzi huo hautaahirishwa,na utaendelea kama ilivyopangwa, tarehe 23 mwezi Desemba.

“ Tunaelekea kwenye uchaguzi hapa hakuna kuahirisha kitu hapa: Endapo tunaahirisha uchaguzi Je? Mwafahamu madhara ambayo yatakuja kutokea" ?

“Vifaa vimehifadhiwa kwenye maghala ya muda, sasa uchaguzi ukiahirishwa nani atalinda vifaa hivyo? Matokeo haya yote yanaonyesha kwamba muda huu Hatuwezi kusimamisha kitu, upande wa CENI.” amesema Jean Pierre Kabamba afisa wa Tume ya Uchaguzi

Rais Joseph kabila aliyemaliza muhula wake tangu mwaka 2016 alizindua kampeni katika mkutano aliouitisha katika shamba lake la Kingakati na kuwataka wafuasi wa muungano wa vyama tawala FCC kuhakikisha mrithi wake Emmanuel Ramazani shadari anapata ushindi.

Lambert Mende, Waziri wa Habari na msemaji wa serikali, anaona kuwa, chama tawala kitapata ushindi mkubwa.

“Tuna uhakika na ujasiri wote kwamba tutashinda uchaguzi huu, tumekuwa katika hali ya mapambano makali, lakini hatuogopi neno lolote kwa sababu tumewaletea wakongomani mambo mengi mazuri tu katika kipindi cha miaka 17,”

“ Naamini hatuwezi kujivunia hayo, ila yabidi tuwe wanyenyekevu wananchi wanalifahamu hilo. Tutashinda uchaguzi na ukitaka kuuona ushindi wetu wewe angalia tu wapinzani wetu, hawana lolote. wameshindwa kujikusanyia umati wa watu, niseme tu kwamba ni panya mwenye kukonda ndiye alizaliwa huko Geneva”. alisema Mende.

Suala muhimu katika uchaguzi huu ni uongozi wa taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini ambalo halijawahi kushuhudia makabidhiano ya amani ya madaraka tangu lilipopata uhuru wake kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960, ambapo hili litashuhudiwa kwa mara ya kwanza katika nchi hiyo.

 

(Kutoka kushoto kwenda kulia) Vital Kamerhe, Felix Tshisekedi, Adolphe Muzito, Moise Katumbi na Jean-Pierre Bemba, wanasiasa wakuu wa upinzani DRC, kabla ya mkutano na waandishi wa habari Septemba 12, 2018 huko Brussels, Ubelgiji.
(Kutoka kushoto kwenda kulia) Vital Kamerhe, Felix Tshisekedi, Adolphe Muzito, Moise Katumbi na Jean-Pierre Bemba, wanasiasa wakuu wa upinzani DRC, kabla ya mkutano na waandishi wa habari Septemba 12, 2018 huko Brussels, Ubelgiji. © AFP

Wagombea zaidi ya 20 wanawania urais nchini humo, lakini hawa ndio wagombea wakuu:-

-Vital Kamerhe- anawania kupitia chama cha UNC.Ni Waziri wa zamani.

-Emmanuel Ramazani Shadary- Mgombea wa chama tawala, Waziri wa zamani wa Mambo ya ndani na Gavana wa zamani wa jimbo la Maniema.

-Felix Tshisekedi- Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani UDPS, mtoto wa mwanasiasa mkongwe marehemu Etienne Tshisekedi

-Martin Fayulu- Mgombea anayeungwa mkono na wasiasa watano wa upinzani akiwemo Jean-Pierre Bemba na Moise Katumbi.