ICC-CAR-ANTI-BALAKA-MAUJI-UHALIFU

Kiongozi wa zamani wa Anti-Balaka afikishwa ICC

Alfred Yekatom kiongozi wa zamani wa kundi la Anti-Balaka katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC mjini Hague Novemba 23 2018
Alfred Yekatom kiongozi wa zamani wa kundi la Anti-Balaka katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC mjini Hague Novemba 23 2018 www.icc-cpi.int

Kiongozi wa zamani wa kundi la waasi la Anti-Balaka nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati Alfred Yekatom, maarufu kama “Colonel Rambo” amefikishwa mbele ya  Mahakama ya Kimataifa ya ICC, mjini Hague nchini Uholanzi.

Matangazo ya kibiashara

Yekatom, mwenye umri wa miaka 43, aliwasili Mahakamani Ijumaa asubuhi akiwa amevalia suti na kuonekana mtulivu huku alisikiliza kwa makini mashtaka 14 ya uhalifu wa kivita yanayomkabili  ikiwemo kuwaajiri watoto katika kundi la Anti-Balaka,

Mshukiwa huyo ambaye ni mbunge, nchini mwake, ameiambia Mahakama kuwa, aliteswa wakati alipokamatwa jijini Bangui, na hakuelezwa sababu yoyote ya kukamatwa kwake.

Kikao cha leo kiilkuwa  cha kumtambua mshukiwa huyo, ambaye amesema amefahamu mashtaka dhidi yake Mahakamani, na hakuwahi kuelezwa ni kwanini anashtakiwa.

Jaji anayeongoza kesi hiyo, Antoine Kesia-Mbe Mindua amesema kwa sasa hawezi kuamua kuhusu madai yake ya kuteswa lakini, akaeleza kuwa mashtaka dhidi yake yatathibitishwa tarehe 30 mwezi Aprili mwaka 2019.

Mahakama ya ICC, ilitoa hati ya kukamatwa kwa Yekatom mwaka 2015, baada ya mapigano kuzuka nchini humo kati ya waasi wa Anti -Balaka na Seleka mwaka 2013.