Al Shabab yadai kuhusika katika shambulio dhidi ya sehemu ya ibada Somalia
Imechapishwa:
Wapiganaji kadhaa wa kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Al Shabab wameendesha shambulio dhidi ya mahali pa ibada katika mji wa Galkayo katikati mwa Somalia Jumatatu wiki hii, na kuua watu 11, afisa wa kundi hilo amesema.
"Gari iliyotegwa bomu iliingia katikati ya makaazi ya mtu aliyemtukana Mtume wa Mungu. Wapiganaji wetu sasa wako ndani ya makazi yao," amesema Abdiasis Abu Musab, msemaji wa operesheni za kijeshi za Al Shabab.
Baadaye, amesema kuwa mchungaji Abdiweli na wafuasi wake kumi wameuawa. Shirika la Habari la Reuters linasema halikuweza kuthibitisha idadi ya watu waliouawa katika shambulio hilo.
Kwa mujibu wa afisa wa mkoa wa Mudug ambaye ameohojiwa na Reuters, Abdiweli alikuwa akitishiwa mara kwa mara na kundi hilo la wanamgambo Waislam.