Washukiwa wa ugaidi wawauwa watu 12 Kaskazini mwa Msumbiji
Imechapishwa:
Watu kumi na wawili wameuawa Kaskazini mwa nchi ya Msumbiji katika shambulizi ambalo linadhaniwa kuwa limetekelezwa na wanamgambo wa kundi la wapiganaji wa Kiislam.
Taarifa kutoka nchini humo zinaeleza kuwa shambulizi hilo limesababisha maelfu ya wananchi wa taifa hilo hasa wale walio katika vijiji, kukimbilia katika nchi jirani ya Tanzania.
Polisi nchini Msumbilji wameeleza mwishoni mwa juma lililopita kuwa shambulizi hilo lilitokea katika kijiji cha Chicuaia Velha karibu na Tanzania na kusababisha mauaji hayo.
Mwandishi mmoja wa kujitegemea amesema kuwa watu hao walikatwa shingo hadi kufa, wakiwa nyumbani kwao.
Hili ni shambulizi la tatu, kwa kipindi cha miezi miwili katika eneo la Cabo Delgado, na kusababisha mauaji ya watu zaidi ya 20.