DRC-SIASA-UPINZANI-UCHAGUZI

Felix Tshisekedi arejea nyumbani na kuanza kampeni za kutafuta kura za urais

Vital Kamerhe na Félix Tshisekedi  wakikaribishwa katika jiji kuu Kinshasa siku ya Jumanne Novemba 27 2018
Vital Kamerhe na Félix Tshisekedi wakikaribishwa katika jiji kuu Kinshasa siku ya Jumanne Novemba 27 2018 REUTERS/Olivia Acland

Kiongozi wa chama cha UPDS Felix Tshisekedi amerejea nyumbani nchini DRC na kuanza kampeni za kutafuta kura, ili kushinda urais wakati wa Uchaguzi Mkuu tarehe 23 mwezi Desemba.

Matangazo ya kibiashara

Wiki iliyopita, Tshisekedi aliafikiana na kiongozi wa chama cha UNC kuunda muungano kuelekea Uchaguzi huo, baada ya kukutana jijini Nairobi nchini Kenya.

Akiwahotubia maelfu ya wafuasi wake jiji Kinshasa siku ya Jumanne, Tshisekedi amesema kuwa, ana uhakika wa kushinda Uchaguzi huo.

“Tutaenda na watu na tutashinda uchaguzi,” amesema Tshisekedi, mwenye umri wa miaka 55, mtoto wa Marehemu Etenne Tshisekedi aliyefariki dunia mwezi Februari mwaka 2017.

Aidha, amewaahidi wafuasi wake kuwa atatuma wajumbe wake katika maeneo yote ya nchi hiyo, kuhakikisha kuwa, hakuna wizi wa kura unaofanyika.

Iwapo Tshisekedi atashinda Uchaguzi huo, Kamerhe atakuwa Waziri Mkuu kwa mujibu wa mkataba huo wa Nairobi.

Wawili hao wiki mbili zilizopita, waliondoa saini zao katika mkataba wa Geneva, ambao pamoja na wanasiasa wengine watano wa upinzani walikuwa wamekubaliana kumuunga mkono Martin Fayulu kuwa mgombea wao lakini, wafuasi wao hawakuridhika.