LIBYA-CHAD-USALAMA

Majirani wa Libya wakutana Khartoum kujadili usalama wa kikanda

Nchi sita jirani na Libya zinakutana Alhamisi wiki hii katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, kujadili kuhusu uratibu wa usalama katika ukanda huo. Mkutano huu wa mara kwa mara utahudhuriwa kwa mara ya kwanza na mawaziri wawili wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa na Italia.

Khartoum, mji mkuu wa Sudan. Picha iliyopigwa usiku (picha ya kumbukumbu).
Khartoum, mji mkuu wa Sudan. Picha iliyopigwa usiku (picha ya kumbukumbu). (CC)/Aamirco/Wikipédia
Matangazo ya kibiashara

Wawakilishi kutoka Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Nchi za Kiarabu pia watakuwapo katika mkutano huo, pamoja na Ghassan Salamé, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Libya. Mkutano huu ni mwendelezo wa mikutano ya awali ya usalama ambayo ilifanyika katika miji ya Ndjamena, Tripoli na Niamey katika miezi ya hivi karibuni.

Hali inayoendelea nchini Libya kwa usalama wa eneo la Sahel, ugaidi, na biashara haramu ya wahamiaji, silaha na madawa ya kulevya ni miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa katika mkutano huounaojumuisha wajumbe kutoka nchi sita jirani na Libya.

Mkutano huu mpya unaojumuisha wizara mbalimbali kutoka nchi hizo sita utajadili pia changamoto za hali ya usalama nchini Libya kuhusu amani na utulivu katika eneo la Sahel na utajaribu kuongeza uratibu wa usalama kati ya nchi husika.

Kuanguka kwa utawala wa Kanali Gaddafi mwaka 2011 umesababisha uwepo wa makundi mengi ya watu wenye silaha kusini mwa Libya. Makundi ambayo yanajihusisha na uhalifu kwenye maeneo ya mipakani.

Shughuli za makundi haya ya watu wenye silaha zinahatarisha usalama na utulivu wa nchi kadhaa kama vile Chad na Niger.

Misri, ambayo inahudhuria mkutano huo, ilisaini mkataba na Sudan siku ya Jumatano (Novemba 28) ili kufanya doria za kijeshi pamoja kwenye mpaka wa nchi hizo mbili na Libya. Mikataba kama hiyo ipo kwa miezi michache kati ya Libya, Chad na Niger, lakini utekelezaji wa mikataba hiyo umechelewa. Mawaziri wamezungumzia ukosefu wa fedha na kutoa wito kwaUmoja wa Ulaya kusaidia.