DRC-UCHAGUZI-SIASA

Kiongozi wa upinzani DRC aishtumu serikali kukwamisha kampeni yake

Novemba 11, 23018 Geneva, Uswisi, Martin Fayulu aliteuliwa kuwa mgombea mmoja wa upinzani nchini DRC katika uchaguzi wa urais wa Desemba 23.
Novemba 11, 23018 Geneva, Uswisi, Martin Fayulu aliteuliwa kuwa mgombea mmoja wa upinzani nchini DRC katika uchaguzi wa urais wa Desemba 23. Fabrice COFFRINI / AFP

Mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya vyama vya upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Lamuka) Martin Fayulu ameishutumu serikali ya DRC kwa kukwamisha kampeni yake anayoendelea kufanya katika maeneo kadhaa.

Matangazo ya kibiashara

Bw Fayulu amesema kuwa mgombea wa upande wa utawala anaendelea kupewa nafasi kubwa na pana ya kuzunguuka kwa uhuru katika kila maeneo nchini humo.

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa kamati ya kampeni ya mgombea huyo, Pierre Lumbi amesema Fayulu amepanga kuelekea Butembo siku ya Jumapili na kisha Beni siku ya Jumatatu, lakini mpaka sasa ndege yake haijaruhusiwa na serikali.

“Ni mbinu ambayo imepangwa katika hali ya ujanja ili mgombea pekee wa upinzani ashindwe kupiga kampeni zake. Tabia hii ya serikali haikubaliki, na ni kinyume na sheria za jamhuri na zaidi sana ni kinyume na taratibu zilizowekwa katika sheria za uchaguzi. Muungano wa Lamuka hautakubali ujanja huo, ” amesema Pierre Lumbi.

Hata hivyo Waziri wa Uchukuzi Jose Makila amekanusha taarifa hiyo na kusema kuwa ofisi yake haijapokea maombi yoyote kutoka kwa mgombea huyo wa upinzani.

“Mimi sijapokea maombi yoyote kutoka kwao, pia lazima kuelewa kwamba kuna utaratibu kwa mtu yeyote anayeleta ndege kutoka nje ya nchi, ili ije kutumiwa kwa muda mfupi katika ardhi ya Congo, lazima utaratibu ufatwe, ” Jose Makila amesema.

Katika hatua nyingine mwanamke pekee anayewania kiti cha urais nchini DRC Marie-Josée Ifoku ameitaka tume ya Uchaguzi (Ceni) kutoegemea upande wowote.

“Leo hii, mnayo nafasi ya kutengeneza sifa yenu, msije kuonekana kwamba nyinyi ni wenye kuegemea upande wowote. Ninawaombeni, komesheni tabia hii ya kumtengenezea mazingira ya kushinda mgombea wa upande wa utawala, ambapo wengine hawapewi haki yoyote,” Marie Ifoku amesema.

Kampeni za uchaguzi unaopangwa kufanyika Desemba 23 mwaka huu, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zilianza Novemba 22 na zitahitimishwa siku 30 baadaye, lakini wagombea wengi wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa pesa, hali ngumu ya maisha lakini pia usalama mdogo maeneo kadhaa hususan mashariki mwa nchi hiyo.