GABON-SIASA-AFYA

Maafisa wakuu wa Gabon wamtembelea Rais Bongo Morocco

Picha rasmi iliyotolewa na serikali ya Morocco ikimuonyesha Mfalme wa Morocco Mohammed VI (kushoto) na Rais wa Gabon Ali Bongo, katika hospitali ya kijeshi ya mji mkuu wa Morocco.
Picha rasmi iliyotolewa na serikali ya Morocco ikimuonyesha Mfalme wa Morocco Mohammed VI (kushoto) na Rais wa Gabon Ali Bongo, katika hospitali ya kijeshi ya mji mkuu wa Morocco. Handout / Moroccan Royal Palace / AFP

Viongozi wakuu nchini Gabon, ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu na Makamu wa rais wamefanya safari kwenda kumjulia hali rais wa nchi hiyo Ali Bongo Ondimba anaendelea kupatiwa matibabu katika mji mkuu wa Morocco, Rabat, kwa mujibu shirika la Habari la AFP likinukuu chanzo rasmi kutoka ikulu ya rais.

Matangazo ya kibiashara

Emmanuel Issoze Ngondet, Waziri Mkuu, Pierre-Claver Maganga Moussavou, makamu wa rais, Mary Magdalena Mborantsuo, Rais wa Mahakama ya Katiba na Brice Lacruche Alihanga, Mkurugenzi katika ofisi ya rais Bongo, waliwasili siku ya Jumatatu usiku nchini Morocco, chanzo hicho kimeongeza.

Ali Bongo, mwenye umri wa miaka 59, aliwasili Alhamisi Novemba 29 katika hospitali ya kijeshi ya Rabat kuendelea kupata matibabu, baada ya zaidi ya mwezi mmoja akilazwa katika hospitali moja mjini Riyadh nchini Saudi Arabia kwa ugonjwa ambao bado haujajulikana rasmi.

Siku ya Jumatatu, Mfalme wa Morocco, Mohammed VI, rafiki wa muda mrefu wa rais wa Gabon, alimtembelea hospitali.

Rais Bongo, anapata mapumziko ya baada ya matibabu kabla ya kurejea jijini Libireville.Ugonjwa unaosumbua, haujawekwa wazi lakini, inaaminika kuwa alipata kiharusi mwishoni mwa mwezi Oktoba, wakati alipokuwa amekwenda nchini Saudi Arabia kuhudhuria mkutano wa kimataifa.

Mnamo Novemba 11, msemaji wa ikulu Ike Ngouoni aliwaambia waandishi wa habari kuwa rais Ali Bongo atakuwa mwenye afya nzuri katika siku za hivi karibuni.

Vyombo vya habari nchini Gabon vilikuwa vikifahamisha kuwa huenda rais Ali Bongo akapelekwa mjini Paris au London.

Ali Bongo ni mtoto wa aliekuwa rais wa zamani wa nchi hiyo Omar Bongo ambae aliongoza taifa hilo tangu mwaka 1967 hadi alipofariki Juni 8 mwaka 2009.