MOROCCO-SAHARA-USALAMA-SIASA

Sahara ya Magharibi: Zaidi ya miaka 40 ya migogoro

Katikati mwa mji wa Laayoune, mji mkuu wa Jamhuri ya Kiarabu ya Sahara Magharibi.
Katikati mwa mji wa Laayoune, mji mkuu wa Jamhuri ya Kiarabu ya Sahara Magharibi. © Bjørn Christian Tørrissen/CC/Wikimedia Commons

Umoja wa Mataifa unakutana Jumatano wiki hii mjini Geneva, nchini Uswisi kujadili hali ya Sahara ya Magharibi. Tangu kuondoka kwa Uhispania, iliyoitawala nchi hiyo katika enzi za ukoloni mnamo miaka ya 1976, eneo hilo linadhibitiwa 80% na Morocco wakati kundi la Polisario Front linaendelea kuomba uhuru wa eneo hilo.

Matangazo ya kibiashara

Mazungumzo, chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa, yamesimama tangu mwaka 2012. Kutokana na hali hiyo Horst Kohler, Mjumbe mpya wa Umoja wa Mataifa kuhusu suala hili, ameamua kufufua mazungumzo kwa kualika wadau wote mjini Geneva, akiwa na matumaini ya kufikia suluhu ya mgogoro huo wa zamani wa zaidi ya miaka 40.

Wadau wanaokutana kwa muda wa siku mbili huko Geneva hawajakutana tangu mwaka 2012 ili kujadili suala la Sahara ya Magharibi. Eneo ambalo hatima yake imekubwa na kiza kwa miaka kadhaa.

Kwa muda mrefu Sahara Magharibi ilikuwa koloni ya Uhispania. Mnamo mwaka 1975, makubaliano yaliyotiliwa saini mjini Madrid yalimaliza utawala huo wa ukoloni na kugawanya eneo hilo mara mbili. Eneo la kusini mwa Sahara Magharibi lilipewa Mauritania, ambayo ilirejesha sehemu hiyo miaka sita baadaye, wakati eneo la kaskazini na katikati lilichukuliwa na Morocco.

Makubaliano yalitiloiwa saini siku chache baada ya maandamano ya amani yaliyoandaliwa na Mfalme Hassan II wakati zaidi ya raia 350,000 wa Morocco walizuru eneo hilo. Tangu wakati huo, hali ya mvutano iliibuka kati ya utawala wa Hassan II na kundi la waasi la Polisario Front.

Polisario Front inaomba uhuru wa Sahara ya Magharibi.

Mnamo mwaka 1976, Polisario Front ilitangaza eneo hilo kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Sahrawi (SADR). Mwaka 1984, ilijiunga na Umoja wa Afrika (ambayo ilikuwa bado ikiitwa OAU) na Morocco kuamua kujiondoa kwenye taasisi hiyo.

Mapigano kati ya pande hizo mbili yaliendelea hadi mwaka wa 1991 wakati mkataba wa usitishwaji mapigano ulipoanza kutumika. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulitumwa nchini na kuandaa kura ya maoni ya kujitawala.

Tangu wakati huo, kura hiyo ya maoni imekuwa ni chanzo cha mvutano kati ya Rabat na Polisario. Mipango kadhaa imeendelea na pande mbalimbali, lakini kila wakati, imekuwa ikifutiliwa mbali.