DRC-UCHAGUZI-USALAMA

Wawili wauawa katika makabiliano na polisi Lubumbashi, DRC

Mgombea urais nchini DRC, Martin Fayulu alipowasili Beni, Desemba 5, 2018 (picha ya kumbukumbu).
Mgombea urais nchini DRC, Martin Fayulu alipowasili Beni, Desemba 5, 2018 (picha ya kumbukumbu). © ALEXIS HUGUET / AFP

Wafuasi wawili wa kiongozi wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameuawa katika makabiliano na polisi mjini Lubumbashi wakati wa mkutano wa kampeni wa mgombea wao Martin Fayulu, mashirika ya kiraia yameripoti.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu nchini DRC, ACAJ, limesema kuwa watu 43 walijeruhiwa wakiwemo watu 15 waliojeruhiwa na risasi wakati wafuasi hao walipokuwa kwenye msafara mjini Lubumbashi, mji wa pili kwa ukubwa nchini humo.

Shirikio hilo limeongeza kuwa miongoni mwa waliojeruhiwa wapo polisi ambao mmoja kati yao hali yake sio nzuri.

Kwa upande wake jeshi la polisi mjini Lubumbashi limedai kuwa maofisa wake 11 walijeruhiwa sambamba na raia wawili ambao ni wafuasi wa mgombea wa upinzani Martin Fayulu.

Hata hivyo muungano wa vuguvugu la upinzani la LAMUKA wenyewe umedai kuwa zaidi ya wafuasi wake 6 waliuawa na polisi.

Haya yanajiri wakati huu zikiwa zimebaki siku 12 pakee kabla ya nchi hiyo kufanya uchaguzi wake mkuu huku kinyang’anyiro kikitarajiwa kuwa kati ya mgombea wa chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary, Martin Fayulu na wagombea wengine wa upinzani Felix Tshisekedi na Vital Kamerhe.