MADAGASCAR-SIASA-UCHAGUZI

Rajoelina aongoza duru ya pili ya Uchaguzi wa urais nchini Madagascar

Andry Rajoelina anaelekea kushinda Uchaguzi wa urais nchini Madagascar
Andry Rajoelina anaelekea kushinda Uchaguzi wa urais nchini Madagascar AFP

Rais wa zamani wa Madagascar Andry Rajoelina anaelekea kurejea madarakani, kwa mujibu wa matokeo ya awali ya duru ya pili ya Uchaguzi wa urais yanayoendelea kutangazwa.

Matangazo ya kibiashara

Tayari kura Milioni 3.5 kati ya Milioni 5 zimehesabiwa na Rajoelina anaongoza kwa asilimia 55.7 dhidi ya mpinzani wake Marc Ravalomanana, ambaye ana asilimia 44.2.

Matokeo ya mwisho yanatarajiwa kutolewa wiki ijayo.

“Tunasubiri matokeo rasmi lakini naamini kuwa, kwa namna mambo yanavyokwenda, ushindi ni wetu,” amesema Hajo Andrianainarivelo, msaidizi wa Rajoelina.

Hata hivyo, Fanirisoa Erinaivo, aliyewania urais katika duru ya kwanza, amesema hawaamini matokeo yanayotangazwa kwa kile anachokieleza kuwa, matokeo waliyonayo kutoka vituo vya kupigia kura, yanaonesha kuwa Marc Ravalomanana, anaongoza.

Ravalomanana anatarajiwa kuzungumzia matokeo hayo siku ya Jumapili, ishara kuwa kutakuwa mzozo baada ya matokeo ya mwisho kutangazwa.

Waangalizi wa Umoja wa Ukaya wanasema, hakuna ushahidi kuwa kumekuwa na wizi wa kura.