DRC-SADC-ICGLR-SIASA-USALAMA

Wakuu wa SADC watiwa wasiwasi mkubwa na hali ya uchaguzi DRC

Wakati wa mkutano wa SADC kuhusu hali ya uchaguzi nchini DRC uliofanyika Brazzaville tarehe 26 Desemba, Kinshasa haikuwakilishwa.
Wakati wa mkutano wa SADC kuhusu hali ya uchaguzi nchini DRC uliofanyika Brazzaville tarehe 26 Desemba, Kinshasa haikuwakilishwa. Reuters/Bouka Roch

Hali ya uchaguzi nchini DRC imejadiliwa kwa kina katika mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Maendelo ya Kiuchumi ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya nchi za Maziwa Makuu (ICGLR). Mkutano ambao ulifanyika katika mji mkuu wa Congo, Brazzaville.

Matangazo ya kibiashara

Wakuu wa nchi hizo wana wasiwasi na hali ya kisiasa inayoendelea nchini humo ikiwa zinasalia tu siku nne kabla ya Uchaguzi Mkuu Jumapili Desemba 30. Uchaguzi ambao tayari umeahirishwa katika maeneo matatu ya nchi hiyo. Beni, Butemb ( mashariki mwa DRC) na Yumbi, (magharibi mwa nchi). Uchaguzi huo ulikokuwa umepangwa kufanyika Desemba 23 uliahirishwa kwa mara ya kwanza hadi Jumapili Desemba 30.

Marais wanne (Angola, Namibia, Zambia, Botswana) walifanya safari kwenda Brazzaville, kwa mwaliko wa Rais Denis Sassou-Nguesso.

Hata hivyo DRC, kwa upande mwingine, haikuwakilishwa.

Katika taarifa yao ya mwisho, marais hao walielezea "wasiwasi wao" baada ya machafuko wakati wa kampeni nchini DRC lakini wametoa ujumbe kwa wadau wote katika mchakato mzima wa uchaguzi kutia mbele maslahi ya nchi na wananchi hasa wakati huu mgumu.

Mawaziri wa Mambo ya nje kutoka muungano wa mataifa ya Kusini mwa bara la Afrika SADC na eneo la Maziwa Makuu, leo watakuwa jijini Kinshasa kukutana na rais Joseph Kabila, kuzungumzia Uchaguzi wa siku ya Jumapili.

Mawaziri hao watamwambia ujumbe wa viongozi wa SADC na ICGLR waliokutana Jumatao wiki hii jijini Brazzaville kuzungumzia uchaguo huo tata.