MADAGASCAR-UCHAGUZI-SIASA

Maandamano ya upinzani yazimwa kwa gesi ya machozi

Wafuasi wa mgombea wa urais wa upinzani Madagascar, Marc Ravalomanana, wakiandamana kwenye eneo maarufu la 13 Mai Plaza, Antananarivo, Desemba 29, 2018.
Wafuasi wa mgombea wa urais wa upinzani Madagascar, Marc Ravalomanana, wakiandamana kwenye eneo maarufu la 13 Mai Plaza, Antananarivo, Desemba 29, 2018. © AFP

Vikosi vya usalama vimesambaratisha maandamano ya upinzani yaliyopigwa marufuku katika mji mkuu wa Madagascar, Antananarivo, Jumatano wiki hii.

Matangazo ya kibiashara

Waandamananji wanaomuunga mkono mgombea urais aliyeshindwa katika uchaguzi wa urais wa Desemba 19 Marc Ravalomanana waliingia mitaani wakipinga dhidi ya "wizi wa kura uliogubika uchaguzi huo".

"Tumekuja kuonyesha wizi mkubwa kubwa na koasoro mbalimbali zilizojitokeza katika duru ya pili ya uchaguzi wa urais uliofanyika hivi karibuni, Lakini tumerushiwa mabomu ya machozi," Kiongozi wa maandamano hayo, ambaye ni mbunge wa chama cha TIM cha Marc Ravalomanana, Hanitra Razafimanantsoa ameviambia vyombo vya Habari.

"Muheshimu chaguo letu, hatukubaliani na uchaguzi uliogubikwa na udanganyifu", hayo ni maeneo yaliyokuwa yameandikwa kwenye mabango yaliyokuwa yakibebelewa na waandamanaji.

Maelfu ya waandamanaji wamekusanyika Jumatano wiki hii lakini walisambaratishwa haraka kwa mabomu ya machozi karibu na eneo la kuu la 13-Mai, lililokuwa limezingirwa na vikosi vya usalama.

Siku ya Jumamosi, maelfu ya wafuasi wa Ravalomanana waliingia mitaani kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais. Maandamano hayo yaliyokuwa yamepigwa marufuku yalifanyika kwa utulivu.

Rais wa zamani wa Madagascar Andry Rajoelina alishinda duru ya pili ya uchaguzi wa urais kwa 55.66% ya kura, na kumshinda mpinzani wake Marc Ravalomanana, aliyepata 44.34% ya kura, kulingana na matokeo yaliyotolewa na Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (CENI).

Lakini wafuasi wa rais wa zamani Marc Ravalomanana wanaomba kufutwa kwa ushindi wa Andry Rajoelina kutokana na "udanganyifu" na "rushwa" kutoka Tume ya Uchaguzi (CENI).

Mahakama ya Katiba (HCC), ambayo ni mahakama ya juu nchini, sasa inatathmini madai ya Ravalomanana na inatarajia kutoa uamuzi wake katikati ya wiki ijayo.