SOMALIA-UN-USALAMA

Somalia yamfukuza mjumbe wa Umoja wa Mataifa

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Nicholas Haysom
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Nicholas Haysom hadalsame.com

Serikali ya Somalia, imemfukuza mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo Nicholas Haysom, kwa madai kuwa anaingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo kwa makusudi.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii ya Somalia imekuja baada ya mjumbe huyo hivi karibuni kukosoa namna maafisa wa usalama nchini humo walivyotumia nguvu kupambana na waandamanaji.

Katikati ya mwezi Desemba mwaka 2018, maafisa wa usalama walipambana na waandamanaji mjini Baidoa, Kusini Magharibi mwa nchi hiyo na kusababisha vifo vya watu 15 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 300.

Waandamanaji walijitokeza kupinga hatua ya serikali, kumkamata Muktar Robow kiongozi wa zamani wa kundi la Al Shabab aliyekuwa anawania urais wa jimbo hilo.

“Mjumbe huyo anayemwakilisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Nicholas Haysom, haruhusiwi tena kuingia nchini Somalia,” taarifa ya Wizara ya Mambo ya nje imesema.

Umoja wa Mataifa haujazungumzia hatua ya serikali ya Somalia kumfukuza mjumbe wake.

Haysom, wakili mwenye uzoefu raia wa Afrika Kusini, na mwanadiplomasia wa siku nyingi, kabla ya kuteuliwa kwake katika nafasi hiyo mwezi Septemba mwaka 2018, aliwahi pia kuhudumu nchini Sudan na Sudan Kusini.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, umekuwa ukisaidia katika juhudi za kuleta amani na kupambana na ugaidi nchini humo.