GUINEA BISSAU-ELIMU-MGOMO

Walimu waendelea na mgomo hadi mwishoni mwa mwezi Januari Guinea Bissau

Chuo cha kidini (madrasa) katika mji wa Gabu, Guinea-Bissau, Desemba 14, 2008.
Chuo cha kidini (madrasa) katika mji wa Gabu, Guinea-Bissau, Desemba 14, 2008. © AP

Walimu nchini Guinea-Bissau, ambao wamekuwa katika mgomo tangu mwezi Septemba mwaka jana, wameamua kuendelea na mgomo hadi mwishoni mwa mwezi Januari 2019.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kushindwa kuafikiana katika mkutano na Wizara ya Elimu.

Kwa miaka kadhaa, walimu nchini Guinea Bissau, nchi maskini Afrika Magharibi, wamekuwa wanadai malipo ya malimbikizo ya mishahara, kupitishwa kwa mpango wa kazi kwa walimu wote, pamoja na kuwekwa katika mazingira bora za kazi.

"Tutaendelea na mgomo mpaka pale madai yetu yatapatiwa suluhu.Tayari tumewasilisha barua ya kufahamisha kwamba tutakuwa na mgomo wa siku thelathini, mgomo ambao utaanza siku ya Jumatatu Januari 7, na barua nyingine itawasilishwa mgomo huo utakapomalizika," amesema kiongozi wa kamati ya waalimu wanaogoma, Bungoma Duarte Sanha, kwa mujibu wa shirika la Utangazaji la VOA.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Julio César Delgado, kwa upande wake amesema katika mkutano na vyombo vya habari kwamba serikali "imechukua hatua muhimu kwa kuanza kwa shule siku ya Jumatatu." "Wakurugenzi wote wa shule wamefahamishwa," Bw Delgado ameongezea, baada ya kukutana na vyama vitatu vya walimu nchini.

Guinea-Bissau, ilitawaliwa na Ureno katika enzi za ukoloni, na ni moja ya nchi za mwisho duniani ukuzingatia ripoti ya Maendeleo ya Binadamu ya Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo (UNDP).

Uchumi wa nchi umebaki tupu na maadhimisho ya miaka 44 ya uhuru wake Septemba 24 yalifanyika bila sherehe yoyote.