GABON-SIASA-USALAMA

Jaribio la mapinduzi lazimwa Gabon

Picha ya askari wakisoma tangazo lao kwenye redio na televisheni ya Gabon, Januari 7, 2019.
Picha ya askari wakisoma tangazo lao kwenye redio na televisheni ya Gabon, Januari 7, 2019. © AFP / YOUTUBE

Jeshi la serikali limefaulu kuzima jaribio la mapinduzi lililokuwa linaendeshwa na kundi la askari wanaodai kuwa ni kutoka kikosi cha ulinzi wa rais. Hali hiyo inatokea wakati Rais wa nchi hiyo, Ali Bongo Ondimba hayupo nchini tangu miezi miwili na nusu ambapo shughuli za serikali zinaendelea kusimamiwa na waziri Mkuu.

Matangazo ya kibiashara

Rais Ali Bongo yupo nchini Morocco akipokea matibabu kutokana na maradhi ambayo hayajafichuliwa baada ya kuugua akiwa ziarani nchini Saudi Arabia Oktoba 24 alipokuwa akihudhuria mkutano mkubwa wa kiuchumi nchini humo.

Waziri wa mawasiliano na msemaji wa serikali amesema wanajeshi waaminifu kwa serikali ya Rais Ali Bongo wamefanikiwa kuzima jaribio la mapinduzi ya serikali nchini humo.

Waziri wa mawasiliano na msemaji wa serikali, Guy-Bertrand Mapangou amesema "kikosi cha askari watano ndio waliendesha jaribio hilo. Wanne tayari wamekamatwa na mmoja yupo mafichoni na atakamatwa saa chache zijazo."

Wanajeshi wenye vifaru na magari ya kivita walikuwa wakishika doria katika barabara za mji mkuu Libreville.

Kundi hilo la askari watano wamekosoa hotuba ya taifa ya rais Bongo wakisema kuwa kumekuwepo na wasiwasi kuhusu uwezo wa Rais Ali Bongo kuongoza nchi ya Gabon.

Hata hivyo msemaji wa serikali amesema mipaka ya nchi inaendelea kufunguliwa.