DRC-SIASA-USALAMA

Uchaguzi DRC: Ceni yawataka raia wa Congo kuwa na subira

Mwenyekiti wa Ceni Corneille Nangaa na maafisa wa Tume ya Uchaguzi, Desemba 20, 2018 Kinshasa.
Mwenyekiti wa Ceni Corneille Nangaa na maafisa wa Tume ya Uchaguzi, Desemba 20, 2018 Kinshasa. REUTERS/Baz Ratner

Tume ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imeahirisha kutangaza matokeo ya awali ya Uchaguzi wa urais, baada ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mwishoni mwa mwaka 2018.

Matangazo ya kibiashara

Tarehe mpya ya kutangazwa kwa uchaguzi haijajulikana. Lakini Tume Huru ya Uchaguzi imesema inafanya kila lililo chini ya uwezo wake ili iweze kutangaza matokeo ya uchaguzi haraka iwezekanavyo kabla ya tarehe 18 Januari 2019, tarehe ambayo ilipangwa kutawazwa kwa rais mpya.

Raia wa DRC walikuwa wamesubiri kutolewa kwa matokeo hayo, siku ya Jumapili Januari 6 kwa mujibu wa ratiba iliyokuwa imetangazwa hapo awali na Tume ya Uchaguzi.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Corneille Nangaa amesema siku ya Jumapili, haikuwezekana kutangazwa matokeo hayo kwa sababu mchakato huo bado haujapatikana.

Hata hivyo amesema Tume ya uchaguzi imeshahesabu asilimia 50 ya kura zilizopigwa.

Tume ya Uchaguzi haijatangaza tarehe ya kutolewa kwa matokeo hayo wakati huu, wananchi wakisubiri matokeo hayo kwa hamu licha ya kuwepo kwa hali ya wasiwasi.

Ushindani mkali unashuhudiwa kuwa kati ya mgombea wa chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary, Martin Fayulu na Felix Tshisekedi wote kutoka upande wa upinzani.

Upinzani unaona kuwa kuchelewa kutangaza matokeo ya uchaguzi ni mbinu za kutaka kuiba kura.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Corneille Nangaa amesema amepata shinikizo kutoka Marekani kuhusu vikwazo vya fedha. Hata hivyo amebaini kwamba vitisho hivyo huenda vikaathiri shughuli nzima ya Tume ya Uchaguzi (CENI).