DRCUNSC-SIASA-USALAMA

Uchaguzi DRC: FCC yadai kuwa mgombea wake ameshinda uchaguzi

Néhémie Mwilanya, Mkurugenzi kwenye ofisi ya Rais wa DRC Joseph Kabila, Mratibu wa FCC.
Néhémie Mwilanya, Mkurugenzi kwenye ofisi ya Rais wa DRC Joseph Kabila, Mratibu wa FCC. youtube.com

Muungano wa vyama vinavyounda Serikali nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, FCC, unasema kuwa mgombea wao wa kiti cha urais Emmanuel Ramazani Shadar ndiye mshindi wa uchaguzi uliofanyika Desemba 30 mwaka jana.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza jana jijini Kinshasa, msemaji wa muungano wa FCC, Emee Kilolo amesema kulingana na matokeo waliyokusanya kutoka kwa mawakala wao yanaonesha kuwa mgombea wao amepata ushindi.

Hata hivyo matamshi haya ya muungano wa FCC yamepingwa vikali na mmoja wa wagombea huru Teodor Ngoy anayehoji uhalali wa matokeo yanayotolewa na muungano wa vyama tawala.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa tume Ya uchaguzi(CENI) Corneille Nangaa amewaambia waandishi wa habari kuwa tume yake itatangaza matokeo kwa mujibu wa sheria na kwamba haifanyi kazi kutokana na mashinikizo ya wanasiasa au watu kutoka nje.

Matamshi ya Nangaa yanakuja wakati ambapo juma lililopita baraza la maaskofu wa kanisa katoliki likidai linajua nani ameibuka mshindi.

Huenda baadhi ya matokeo yakaanza kutangazwa juma hili na tume ya uchaguzi.