Zaidi ya waandamanaji 800 wakamatwa Sudan
Imechapishwa:
Watu zaidi ya 800 wamekamatwa nchini Sudan tangu kuanza kushuhudiwa kwa maandamano ya nchi nzima kuipinga Serikali mwezi Desemba mwaka jana, imesema taarifa ya wizara ya mambo ya ndani ya Khartoum.
Tangazo hili la Serikali limekuja wakati huu ambapo mamia ya wafuasi wa rais Omar al-Bashir wamefanya mkutano mkubwa mjini Khartoum kuonesha uungaji mkono wao kwa Serikali.
Sudan ambayo inakabiliwa na mdororo wa kiuchumi imekumbwa na hali ya sintofahamu tangu tarehe 19 Desemba kufuatia maandamano ya kupinga kupanda kwa bei ya mkate na uhaba wa bidhaa mbalimbali mahitajio.
Maandamano hayo yalibadili mwelekeo na kuwa mandamano ya kupinga utawala wa Omar Al Bashir ambaye alichukuwa madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi mnamo mwaka 1989.
Akiwa mbele ya bunge, waziri wa mambo ya Ndani wa Sudan, Ahmed Bilal Osmane, amesema "waandamanaji 816 wamekamatwa" tangu kuanza kwa maandamano hayo ambayo yameathiri miji kadhaa ikiwa ni pamoja na mji mkuu wa Sudan, Khartoum.
"Maandamano hayo yalianza kwa amani, lakini wahuni wenye nia mbaya walitumia maandamano hayo kwa kupora na kufanya uharibifu," amesema waziri Osmane, huku akiongeza kuwa hali sasa imekuwa tulivu.
Mamlaka zinasema watu 19 ndio wamepoteza maisha hadi sasa kutokana na maandamano hayo, lakini mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema watu 37 ndio waliopoteza maisha.