DRC-UCHAGUZI-SIASA-USALAMA

Martin Fayulu adai kuibiwa kura

Mgombea wa muungano wa upinzani Lamuka, Martin Fayulu wakati wa kampeni yake Goma, Desemba 6, 2018.
Mgombea wa muungano wa upinzani Lamuka, Martin Fayulu wakati wa kampeni yake Goma, Desemba 6, 2018. REUTERS/Samuel Mambo

Baada ya Tume ya Uchaguzi nchini DRC (CENI) kumtangaza Felix Tshisekedi, mwanae Etienne Tshisekedi, mshindi wa uchaguzi wa urais nchini humo, mgombea mwengine wa upinzani Martin Fayulu amesema hakubaliani na matokeo hayo yaliyotangazwa na CENI.

Matangazo ya kibiashara

Bw Fayulu anadai kuwa amefanyiwa unyonge na ana imani kuwa yeye ndiye ameshinda uchaguzi wa urais uliofanyika Desemba 30 mwaka jana.

Mahakama ya Katiba ndio itatangaza matokeo kamili ya uchaguzi wa urais baada ya kutathmini madai ya wagombea wengine ambao hawakubaliani na matokeo hayo ya uchaguzi. Matokeo kamili yanatarajiwa kutangazwa Januari 15 na rais mpya ataapishwa siku tatu baadaye.

Katika mahojiano na RFI, Martin Fayulu, mgombea wa muungano wa upinzani Lamuka, ambaye amechukuwa nafasi ya pili akipata asilimia 34 ya kura amelaani kile alichokiita "mapinduzi ya uchaguzi" na "matokeo ya aibu" ambayo hayahusiani na ukweli wa uchaguzi.

Bw Faylu ameishtumu Tume ya Uchaguzi na mwenyekiti wake Corneille Nangaa akisema kuwa walikula njama ya kumuangusha katika uchaguzi huo ili asionekani mshindi wa uchaguzi.

"Matokeo haya hayahusiani na ukweli wa uchaguzi. Kwa hiyo ninaomba Cenco, Kanisa la Kristo hapa DRC, Symocel na wote ambao walifuatilia uchaguzi kuniambia ukweli, na kutoa matokeo halisi (...) Wameiba ushindi wa wananchi wa DRC na wananchi wa DRC hawatakubali ushindi wao uibiwe, " amesema Martin Fayulu, mgombea wa muungano wa upinzani wa Lamuka.

Huu ni ushindi wa kihistoria kwa chama kongwe cha upinzani nchini DRC, UDPS, na Felix Tshisekedi Tshilombo mwenyewe.

Bw Tshisekedi atakuwa mgombea wa kwanza kabisa wa upinzani kushinda uchaguzi wa urais tangu DRC ilipojipatia uhuru.