DRC-SADC-SIASA-USALAMA

DRC: Wanasiasa watoa misimamo yao kufuatia wito wa SADC

Mkutano wa SADC kuhusu hali ya uchaguzi nchini DRC, Desemba 2018 (picha ya kumbukumbu).
Mkutano wa SADC kuhusu hali ya uchaguzi nchini DRC, Desemba 2018 (picha ya kumbukumbu). Reuters/Bouka Roch

Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC, imetoa wito wa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya kuendelea kwa mzozo kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais wa Desemba 30.

Matangazo ya kibiashara

Tangazo hili limewashangaza wengi. Lakini wanasiasa mbalimbali nchini DRC wametoa misimamo yao kuhusu wito huo wa SADC.

Rais wa Jumuiya ya Maendelea ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC ametoa wito wa kuundwa kwa serikali ya umoja nchini DRC.

Kwa upande wa muungano wa Rais Kabila (FCC), wamesema wamepokea taarifa hiyo kwa tahadhari. "Bado tunachunguza" ukweli "wake," Kodjo Ndukuma, mmoja wa wasemaji wa FCC, amesema siku ya Jumapili usiku. Kwa kuzingatia kwamba waraka huo ulisainiwa na mshauri wa rais wa Zambia anayehusika na masuala ya mahusiano badala ya Namibia, ambayo ndio sasa inaongoza SADC.

Hata hivyo Kodjo Ndukuma amejibu kwamba mgogoro wa uchaguzi ni wajibu wa Mahakama ya Katiba.

"Hakuna muungano wa kisiasa wala mamlaka yoyote kutoka nje ya nchi ambao wanaweza kutoa maagizo yoyote, " ameongeza Kodjo Ndukuma.

Kwa upande wa muungano wa upinzani Lamuka wamekaribisha wito huo. Katika ukurasa wake wa Twitter Martin Fayulu, "amekaribisha" wito huo wa SADC kwa kuwa imeomba "kuhesabu upya" kura ili mtu aliye shinda kweli uchaguzi aweze kutangazwa kuwa rais. Martin Fayulu amebaini kwamba "itakuwa hatari kama hakutakuwa na uungwaji mono kwa mchakato wa kidemokrasia nchini DRC". Hata hivyo hakuzungumzia kuhusu serikali ya umoja wa kitaifa. Lakini Eve Bazaiba, msemaji wake wakati wa kampeni za uchaguzi, amesema: "Tunachotaka tu ni ukweli wa uchaguzi."

Kwa upande wa muungano mwingine wa upinzani CASH wa Felix Tshisekedi ambaye hataki kuzungumza tangu Ceni ilipomtangaza mshindi wa uchaguzi, amejizuia kutoa maoni yoyote kuhusu wito huo.

Kwa upande wa Lucha, Fred Bauma, mmoja wa waanzilishi wa shirika hilo la kiraia, amesema "ni muhimu kwamba SADC" inaomba "kura zihesabiwe upya" ili "ukweli wa uchaguzi ujulikane." Bila hili, Fred Bauma ameongeza "njia yoyote ile itakuwa kinyume cha sheria na itaendelea kuzidisha mdororo wa usalamatunaoshuhudia kwa sasa".

Kwa upande mwingine, amebaini kwamba "serikali za umoja wa kitaifa hazijawahi kuwa suluhisho nchini DRC" na hazijawahi "kutatua kitu chochote" ama kwa uhalali wa utawala, au kwa kutatua matatizo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Kwa upande wa Stéphanie Wolters kutoka Taasisi ya Pretoria ya Mafunzo ya Usalama nchini Afrika Kusini, anasema wito wa SADC haueleweki na jumuiya hiyo inajikanganya kwa taarifa yake.