DRC-AU-SADC-ICGLR-SIASA-USALAMA

AU yaomba kusitishwa kutangazwa matokeo ya mwisho ya Uchaguzi DRC

Rais wa sasa wa Umoja wa Afrika Paul Kagame wakati wa mkutano kuhusu DRC, Alhamisi Januari 17, 2019.
Rais wa sasa wa Umoja wa Afrika Paul Kagame wakati wa mkutano kuhusu DRC, Alhamisi Januari 17, 2019. © EDUARDO SOTERAS / AFP

Umoja wa Afrika umeomba kusitishwa kutangazwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa urais ambao unaendelea kuibua maswali mengi nje na ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Matangazo ya kibiashara

Suala la matokeo ya uchaguzi wa urais nchini DRC limeendelea kuzua hali ya sintofahamu nchini DRC.

Rais wa Umoja wa Afrika Paul Kagame amekutana siku ya Alhamisi na viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu (ICGLR). Mkutano huo ulifanyika kwa faragha na ulidumu karibu saa tano.

Katika taarifa yao ya mwisho wameomba mamlaka nchini DRC kusitisha mpango wa kutangaza matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa urais.

Mahakama ya Katiba inatarajia kutangaza leo Ijumaa matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa urais wa Desemba 30, 2019.

Viongozi wa AU, SADC na ICGLR wamebaini kwamba kuna "mashaka makubwa kwa matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais na ule wa wabunge na magavana wa mikoa" yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi (CENI).

Viongozi hao wamesema wanatarajia kutuma "ujumbe wa ngazi ya juu" mjini Kinshasa kukutana na mamlaka husika.

Ujumbe huo utaundwa na rais wa sasa Umoja wa Afrika Paul Kagame, Mwenyekiti wa sasa wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, na viongozi wengine ambao walihudhuria mkutano huo.

Ujumbe huo unatarajia kujielekeza mjini Kinshasa siku ya Jumatatu wiki ijayo.

Martin Fayulu, mgombea urais aliyeshindwa katika uchaguzi huo ambaye anadai alishinda lakini aliibiwa kura, amekaribisha hatua hiyo ya viongozi wa Umoja wa Afrika, SADC na ICGLR, akisema kuwa ni hatua ambayo inaleta matumani.