DRC-AU-UCHAGUZI

Umoja wa Afrika waahirisha ziara ya ujumbe wake DRC

Rais wa sasa wa Umoja wa Afrika Paul Kagame na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat katika mkutano kuhusu ya hali nchini DRC, Addis Ababa, Januari 17, 2019.
Rais wa sasa wa Umoja wa Afrika Paul Kagame na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat katika mkutano kuhusu ya hali nchini DRC, Addis Ababa, Januari 17, 2019. © REUTERS/Tiksa Negeri

Umoja wa Afrika (AU) umeahirisha ziara ya ujumbe wake iliyokua imepangwa kufanyika Jumatatu mjini Kinshasa, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), baada ya Mahakama ya Katiba kumtangaza Felix Tshisekedi kuwa rais wa DRC siku ya Jumamosi usiku.

Matangazo ya kibiashara

"Tume ya Umoja wa Afrika imepokea tangazo la Mahakama ya Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuhusu matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa urais, uchaguzi wa Bunge na uchaguzi wa Magavana wa Desemba 30, 2018," Umoja wa Afrika umesema katika taarifa yake.

Mahakama ya Katiba ilisahihisha ushindi wa Felix Tshisekedi dhidi ya mgombea mwengine wa upinzani Martin Fayulu, ambaye anapinga matokeo ya uchaguzi, na mgombea wa chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary.

"Ikumbukwe kwamba ziara ya ujumbe wa ngazi ya juu wa Au nchini DRCiliyokuwa imepangwa kufanyika tarehe 21 Januari 2019 imeahirishwa," taarifa hiyo imeongeza.

Ujumbe huo ungeliongozwa na rais wa sasa wa Umoja wa Afrika, Rais wa Rwanda Paul Kagame, na Mwenyekiti wa Tume ya AU, Moussa Faki Mahamat.

Siku ya Alhamisi wiki iliyopita wajumbe wa Umoja wa Afrika waliitaka mamlaka nchini DRC "kusitisha" kutangaza matokeo kamili ya uchaguzi, wakibaini kwamba matokeo ya Tume ya Uchaguzi (CENI) kwa kumtangaza mshindi Felix Tshisekedi yaligubikwa na "udanganyifu mkubwa".

Lakini Mahakama ya Katiba ilipuuzia mbali ombi hilo na usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili, ulifutilia mbali madai ya Martin Fayulu na kutangaza Felix Tshisekedi kuwa rais wa tano wa DRC.