CHAD-MINUSMA-MALI-USALAMA

Walinda amani 10 kutoka Chad wauawa katika shambulio Mali

Askari wa Minusma (picha ya kumbukumbu).
Askari wa Minusma (picha ya kumbukumbu). © AFP/Sebastien Rieussec

Askari 10 wa Umoja wa Mataifa (Minusma) kutoka Chad wameuawa na wengine zaidi ya 25 wamejeruhiwa katika shambulio lililotokea katika eneo la Aguelhok, kilomita 250 Kaskazini mwa Kidal, Kaskazini Mashariki mwa Mali.

Matangazo ya kibiashara

Kundi la kijihadi la Aqmi, lenye mafungamano na kundi la Al-Qaeda limekiri kuhusika na shambulio hilo. Shambulio hilo limetokea siku ya Jumapili. Wakati huo huo Ufaransa imetangaza kuanza kwa operesheni za kikosi cha kimataifa kutoka nchi za ukanda wa Sahel (G5 Sahel).

Walinda amani kumi kutoka Chad wameuawa na wengine zaidi ya 25 wamejeruhiwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema katika taarifa yake.

Ripoti ya awali iliripoti kuwa walinda amani nane wa waliuawa.

Kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Aqmi lenye mafungamano na Al-Qaeda limekiri kuhusika na shambulio hilo, likibaini kwamba limefanya hivyo "katika hatua ya kupinga ziara ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu nchini Chad siku ya Jumapili," kwa mujibu wa shirika la habari la Mauritania la Al-Akhbar , linalofahamika kwa kupokea na kuchapisha mara kwa mara taarifa za kundi hilo.

Mapema Alfajiri, kikosi cha askari wa Umoja wa Mataifa kutoka Chadwanaopiga kambi katika eneo la Aguelhok, kilomita 200 kutoka kwenye mpaka wa Algeria walizima shambulio lililozinduliwa na wauaji waliowasili kwenye magari mengi huku wakijihami kwa silaha za kivita" ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali (Minusma) umesema.

"Wauaji wengi waliuawa katika shambulio hilo hata kama Umoja wa Mataifa ulipoteza askari wake kadhaa, " Minusma imeeleza katika taarifa yake.

Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Mali ambacho kinasimamia amani nchini humo tangu mwaka 2013, baada ya eneo la kaskazini mwa nchi hiyo kuanguka chini ya udhibiti wa kundi la kijihadi lenye mafungamano na al-Qaeda, Minusma, ambayo ina askari na polisi 12,500, tayari imepoteza walinda amani zaidi ya 160.

Shambulio la Jumapili ndiyo shambulio baya zaidi kuwahi kukikumba kikikosi cha Umoja wa Mataifa nchini humo.