SUDAN-HAKI-UCHUMI

Mwanafunzi aliyehukumiwa kifo aachiliwa huru Sudan

Waandishi wa habari wa Sudan wakiandamana dhidi ya hatua zinazominya uhuru wa vyombo vya habari, Khartoum, Sudan, Novemba 15, 2017.
Waandishi wa habari wa Sudan wakiandamana dhidi ya hatua zinazominya uhuru wa vyombo vya habari, Khartoum, Sudan, Novemba 15, 2017. © AFP

Mahakama ya Sudan imemfutia mashitaka na kuamuru kuachiliwa huru mwanafunzi mmoja wa Chuo Kikuu cha Khartoum aliyeshtumiwa kumuua polisi wakati wa maandamano ya mwaka 2016.

Matangazo ya kibiashara

Wakati wa kesi yake ya mwanzo alihukumiwa kifo, kwa mujibu wa shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International.

Asim Omer, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Khartoum, alikamatwa mwezi Desemba 2016 na kushtakiwa kwa mauaji ya polisi wakati wa makabiliano kati ya mamia ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Khartoum na vikosi vya usalama mwezi Aprili 2016.

Asim Omer ambaye ni mfuasi wa chama cha Popular Congress Party (PCP), ambacho kinashiriki serikalini, alihukumiwa kifo mnamo mwezi Septemba 2017. Uamuzi huo wa mahakama ulizua maandamano makubwa ya wanafunzi wa Chuo Kikuu hicho mbele ya mahakama. Maandamano ambayo yalisambaratishwa na vikosi vya usalama kwa kutumia gesi ya machozi.

Awali Mahakama ya Rufaa aliamuru kesi hiyo irejelewa upya, na Jumanne wiki hii, mahakama ilimfutia mashitaka Asim Omer na kuamuru aachiliwe huru, kwa mujibu wa Amnesty International na taarifa ya chama cha PCP.

Amnesty International imekaribisha uamuzi huo, huku ikitolea wito mamlaka kuchunguza madai kwamba Asim Omer "aliteswa gerezani".

"Pamoja na kuwa Asim Omer ameachiliwa huru, haki itakuwa imetendeka ikiwa wale walio husika na maovu hayo watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria," amesema Joan Nyanyuki, Mkurugenzi wa Amnesty International katika Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika.

Sudan inakabiliwa na wimbi la maandamano tangu Desemba 19, 2018. Maandamano yalisababishwa na kuongezwa mara dufu kwa bei ya mkate katika nchi hii inayokabiliwa na mdororo wa kiuchumi.