DRC-RAIS-MPYA-KATIBA-AMANI

Felix Tshisekedi aapishwa kuwa raia mpya wa DRC

Rais mpya wa DRC Felix Tshisekedi
Rais mpya wa DRC Felix Tshisekedi www.rfi.fr

Felix Tshisekedi ameapishwa kuwa rais mpya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika tarehe 30 mwezi Desemba mwaka 2018.

Matangazo ya kibiashara

"Mimi Tshisekedi, Felix Tshilombo Antoine, naapa kuwa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo," alisema huku akishangiliwa na maelfu ya raia wa nchi hiyo jijini Kinshasa.

Amemrithi Joseph Kabila ambaye ameondoka madarakani baada ya kuwa madarakani miaka 17.

Imekuwa mara ya kwanza nchi hiyo kushuhudia mabadiliko ya madaraka kwa amani, kutoka rais mmoja kwenda mwingine, tangu ilipopata uhuru mwaka 1960.

Licha ya kuingia madarakani, Tshisekedi mwenye umri wa miaka 55, anaanza kazi kubwa ya kuongoza nchi hiyo yenye utajiri mkubwa rasimali, lililogawanyika kisiasa.

Katika hotuba yake, rais Tshisekedi ameahidi kuliunganisha taifa hilo na kuhakikisha kuwa amani inarejea lakini pia uchumi unaimarika.

Wakati wa hotuba yake, alilazimika kuikatisha baada ya kuugua ghafla jukwani lakini, baada ya muda mfupi akarejea tena na kuendelea na hotuba yake.

Martin Fayulu, aliyewania urais kupitia muungano wa Lamuka, anaamini kuwa alishinda Uchaguzi huo na hatambui ushindi wa Tshisekedi kwa sababu aliibiwa kura.

Viongozi wa Kanisa Katoliki, walisusia sherehe hizo , kwa kile walichosema kuwa hawaamini kuwa Tshisekedi alishinda Uchaguzi huo.