DRC-SIASA-USALAMA

Tshisekedi kuchukua mikoba ya Kabila

Rais Mteule wa DRC, Félix Tshisekedi (kushoto) na rais anaye maliza muda wake Joseph Kabila.
Rais Mteule wa DRC, Félix Tshisekedi (kushoto) na rais anaye maliza muda wake Joseph Kabila. AFP/John WESSELS

Kwa mara ya kwanza katika historia yake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inatarajia kushuhudia tukio kubwa la kukabidhiana madaraka kwa amani kati ya mtoto wa Etienne Tshisekedi (Felix Tshesekedi) na mtoto wa Laurent Desire Kabila (Joseph Kabila).

Matangazo ya kibiashara

Sherehe zinatarajiwa kufanyika leo alhamisi saa sita mchana (saa za Kinshasa) katika makao makuu ya Bunge.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka wizara ya mambo ya Nje ya DRC, marais kumi na saba kutoka nchi za Afrika , wanatarajia kuhudhuria tukio hilo la kihistoria nchini DRC. Ufaransa na baadhi ya nchi kadhaa za Ulaya zitawakilishwa na mabalozi wao.

Hata hivyo marais wawili wa nchi jirani, Paul Kagame wa Rwanda na Edgar Lungu wa Zambia ambao walitilia mashaka matokeo ya uchaguzi wa urais wa Desemba 30 mwaka 2018,  hawatohudhuria sherehe hiyo.

Zoezi hilo la kukabidhiana madaraka linahitimisha miaka 18 ya utawala wa Joseph Kabila Kabange, ambaye alichukua madaraka baada ya kifo cha baba yake Laurent Desire Kabila (Mzee) ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi katika ukulu ya kinshasa Januari 16, 2001.

Hatimaye Felix Antoine Tshilombo Tshisekedi anakuwa rais wa tano wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, akichukuwa mikoba ya mtangulizi wake Joseph Kabila ambaye anamaliza muda wake.

Felix Tshisekedi alishinda uchaguzi kwa asilimia 38, kulinagana na matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi (CENI) na kuthibitishwa na Mahakama ya Katiba.

Hata hivyo Martin Fayulu, mgombea urais mwengine wa upinzani aliyeshindwa, ambaye anaendelea kudai kuwa alishinda uchaguzi huo licha ya kuibiwa kura, amesema kame hatomtambua Felix Tshisekedi kama rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.