ZIMBABWE-MAANDAMANO-SIASA

Zimbabwe: Upinzani washtumu utawala wa sasa kuwa mbaya zaidi kuliko ule wa Mugabe

Mchungaji Evan Mawarire akikamatwa na polisi wa Zimbabwe Januari 16, 2019 Harare.
Mchungaji Evan Mawarire akikamatwa na polisi wa Zimbabwe Januari 16, 2019 Harare. ©REUTERS/Philimon Bulawayo/File Photo

Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe MDC kimelaani vikali ukandamizwaji ulioshuhudiwa wakati wa kuzimwa kwa maandamano kupinga kupanda kwa bei ya mafuta nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa mashirika ya mawakili kwa ajili ya haki za binadamu, zaidi ya watu 800 walikamatwa wakiwemo wafuasi wa upinzani na wale wa mashirika ya kiraia.

Katika mkutano na waandishi wa habari Jumanne, Januari 29, Chama kikuu cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC), kimelaani ukandamizaji wa siku za hivi karibuni nchini Zimbabwe. Ukandamizaji uliosababisha vifo kufuatia maandamano dhidi ya kupanda kwa bei ya mafuta wiki mbili zilizopita.

Watu zaidi ya 800 walikamatwa kwa mujibu wa Chama cha Wanasheria wa Haki za Binadamu kinaojumuisha wanaharakati, mashirika ya kiraia na wanasiasa wa upinzani.

Kwa upande wa upinzani, ukandamizaji wa siku za hivi karibuni ni tofauti na hauhusiani na mgomo wa wiki mbili zilizopita.

Vikosi vya usalama vinashutumiwa kuendesha operesheni zao usiku katika maeneo yenye makaazi, huku wakiwakamata na kuwapiga raia wasio kuwa na hatia na kuwafanyiwa vitendo vya dulma wanawake.

Chama kikuu cha upinzani cha MDC kimeshtumu mbinu zilizotumiwa katika operesheni hiyo ambazo ni kikatili zaidi kuliko wakati wa Robert Mugabe.

Kwa mujibu wa kiongozi wa chama cha MDC, Nelson Chamisa, serikali inatafuta kuangamiza upinzani wa kisiasa.

"Ni muungano wa wafanyakazi, ZCTU, ambao uliitisha maandamano hayo. Upinzani hauhusiki. Ni uongo mtupu kusema kwamba MDC iliandaa maandamano hayo. Na bado tunaendelea kulengwa. Zaidi ya wabunge wetu arobaini wamefanyiwa vitendo vya udhalili, wengine wamefanyiwa vitisho. Na sita wamekamatwa. Wamekamatwa kwa sababu ya kuwa ni upande wa upinzani. Kuwa katika upande upinzani leo ni uhalifu, " amesema.

Kiongozi wa MDC ameshtumu jumuiya ya kimataifa kusalia kimya, hasa jumuiya ya kikanda, SADC.

Kwa upande wa serikali ya Zimbabwe, unashtumu upinzani kuandaa maandamano hayo na kuchochea vurugu .