DRC-SIASA-UCHAGUZI-USALAMA

Uchaguzi wa wabunge kufanyika Machi 31 Beni, Butembo na Yumbi

Corneille Nangaa Yobeluo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi DRC (CENI), Kinshasa, Januari 10, 2019.
Corneille Nangaa Yobeluo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi DRC (CENI), Kinshasa, Januari 10, 2019. © AFP

Tume ya Uchaguzi nchini DRC (CENI) imetangaza kwamba uchaguzi wa wabunge utafanyika katika maeneo ya Beni Butembo na Yumbi tarehe 31 Machi 2019.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huo umechukuliwa katika mkutano wa Tume ya Uchaguzi CENI Jumatatu wiki hii. Uchaguzi Mkuu haukuweza kufanyika katika maeneo hayo Desemba 30, 2018.

Sababu ya kuahirishwa kwa uchaguzi huo katika maeneo ya Beni, Butembo na Yumbi ilikuwa ni mlipuko wa ugonjwa wa Ebola huko Beni na Butembo, na katika eneo la Yumbi ilitokana na suala la mdororo wa usalama.

"CENI (Tume ya Uchaguzi ya Taifa ya Uchaguzi) imefanya kazi yake kwa kuweka ratiba kwa maeneo haya (Machi 31). Sasa, kazi kubwa itakuwa kwa wale wanaohusika na afya na vikosi vya usalama kutekeleza majukumu yao, " afisa wa mawasiliano wa CENI, Jean-Baptiste Itipo ameiambia VAO Afrique.

Ingawa Machi 31 iliamuliwa kwa uchaguzi wa wabunge, kikao cha CENI pia kimeamua kuwa tume mbalimbali zitatumwa katika maeneo hayo kuchunguza hali inayojiri.

Ugonjwa wa Ebola tayari umeua watu 481 tangu mwezi Agosti mwaka jana katika eneo la Beni mashariki mwa DRC. Ilikuwa sababu ya kuahirishwa kwa uchaguzi katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na Butembo.

Yumbi, inayopatikana magharibi mwa nchi, ilikumbwa na mapigano ya kikabila yaliyosababisha vifo vya watu karibu 900, kwa mujibu wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu nchini DRC.

Uchaguzi wa urais hautafanyika katika maeneo hayo kutokana na kwamba mshindi alitangazwa na tayari ameshakula kiapo.