NIgeria_UCHAGUZI-SIASA

Uchaguzi wa urais Nigeria kufanyika Jumamosi Februari 16

Bango la kampeni la rais anaye maliza muda wake Muhammadu Buhari na mpinzani wake mkuu Atiku Abubakar.
Bango la kampeni la rais anaye maliza muda wake Muhammadu Buhari na mpinzani wake mkuu Atiku Abubakar. REUTERS/Afolabi Sotunde

Wananchi wa Nigeria wanatarajia kupiga kura Jumamosi Februari 16 katika Uchaguzi Mkuu. Watapiga kura kumchagua kati ya Muhammadu Buhari au mgombea mwingine. Muhammadu Buhari, rais wa sasa, anawania muhula wa pili.

Matangazo ya kibiashara

Kuna wagombea zaidi ya 70 ambao wanataka kumng'oa madarakani rais Muhammadu Buhari, lakini ni Atiku Abubakar pekee ambaye mwenye ubavu.

Mwaka 2015, Bw Buhari alichaguliwa baada ya kuahidi kutokomeza kundi la Boko Haram, kupambana dhidi ya rushwa na kuimarisha uchumi. Mshindani mkubwa wa Buhari ni Atiku Abubakar, mwenye umri wa miaka 72.

Rais anayemaliza muda wake Muhammadu Buhari ambaye anawania muhula wa pili wa urais, atalazimika kutotumia ajenda yake iliomsaidia kushinda uchaguzi uliopita wa ahadi ya kuwa na mwanzo mpya.

Wakati huo alikuwa akionyesha fagio jipya, nembo ya chama chake.

Alikuwa hajachaguliwa kidemokrasia licha ya kujaribu mara tatu na sura yake kama mtu asiye mfisadi na mwenye nidhamu ilijitokeza alipokuwa kiongozi wa jeshi katika kipindi cha miezi 20 miaka ya 80.

Alifanya kampeni kama mwanademokrasia mpya, akiapa kukabiliana na ufisadi, kufufua uchumi na kuwashinda wapiganaji wa kundi la Boko Haram.

Naye mshindani wake mkuu Atiku Abubakar ni mtu maarufu nchini Nigeria kwenye nyanja za kisiasa na biashara.

Amefikia moja ya cheo kikubwa kabisa cha utumishi, makamu wa raisi, na pia ni tajiri mkubwa aliyenufaika na sekta ya mafuta.

Abubakar ni mgombea kupitia chama cha People's Democratic Party (PDP), ambacho kimekuwa na ushawishi mkubwa kwa miongo miwili iliyopita. Alikuwa ni afisaa wa PDP pindi chama hicho kilipoundwa wakati wa ukomo wa utawala wa kijeshi. Kupitia chama hicho amehudumu kwa mihula miwili kama makamu wa raisi.

Ofisi kubwa zaidi ya nchi hiyo, urais, umekuwa ukimpiga chenga. Ameshajaribu mara tatu kabla na kuangukia pua.

Jumamosi Februari 16, kwa mara nyengine tena, mwanasiasa huyo mwenye miaka 72 anatupa karata yake, akiwaahidi wananchi kuwa uzoefu wake katika siasa na biashara ni dawa ya changamoto za nchi.

Hata hivyo wakosoaji wake wanamhusisha na kashfa za matumizi mabaya ya fedha, na kudai hilo tu linatosha kumfanya asipewe hatamu katika nchi ambayo rushwa ni tatizo kubwa.

Amekanusha vikali tuhuma hizo akidai zina mkono wa siasa ndani yake.

Endapo atachaguliwa, changamoto kuu mbele yake zitakuwa ongezeko kubwa la ukosefu wa ajira, umasikini wa kutupwa, bunge lililotawaliwa na matabaka ya kikanda, na uchumi unaoyumba kutokana na kutegemea pakubwa sekta ya mafuta.

Amekuwa akipiga kampeni ya kujitofautisha na rais wa sasa, Buhari, ambaye amekuwa akilalamikiwa kwa shidaa za kiuchumi.

Wanaompinga Buhari wanadai kuwa kaliba yake ya kubana matumizi, kutokubali mabadiliko kumekuwa ni kikwazo katika kuingoza na kuleta mabadiliko nchini Nigeria.

Wakosoaji wa bwana Buhari pia wanasema kuwa misimamo iliowavutia watu na kumpigia kura ndio imeonekana kuwa mambo yanayomgeukia.