NIGERIA-UCHAGUZI-SIASA

Uchaguzi Nigeria: Tume ya Uchaguzi matatani

Tume ya Uchaguzi (INEC) yafanya mkutano na waandishi wa habari kuhusu kuahirishwa lkwa uchaguzi NIgeria. Anayesimama mbele ni Mwenyekiti wa INEC, Mahmood Yakubu.
Tume ya Uchaguzi (INEC) yafanya mkutano na waandishi wa habari kuhusu kuahirishwa lkwa uchaguzi NIgeria. Anayesimama mbele ni Mwenyekiti wa INEC, Mahmood Yakubu. © REUTERS/Gbemileke Awodoye

Wengi wanajiuliza kuhusu hatima ya tume ya Uchaguzi nchini Nigeria (INEC) baada ya kuchukuwa hatua ya kusogeza mbele uchaguzi. Uchaguzi uliotarajiwa kufanyika Jumamosi Februari 16 uliahirishwa kwa juma moja hadi Jumamosi Februari 23.

Matangazo ya kibiashara

Wakati huo huo mvutano umeendelea kuongezeka kati ya vyama vikuu vinavyoshtumiana kutaka kuvuruga uchaguzi wa Jumamosi, huku mashirika ya kiraia yakijiuliza kuhusu hatima Tume ya Uchaguzi (INEC).

Kuahirishwa kwa Uchaguzi Mkuu kwa juma moja kumewashangaza wengi, lakini hakuna jipya. Tume ya Uchaguzi sio mara yake ya kwanza, ni kawaida yake, amesema Idayat Hassan, mkurugenzi wa shirika linalofuatilia na kutetea Demokrasia na Maendeleo, shirika lenye makao yake makuu jijini Abuja.

"Imekuwa sasa ni tabia mbovu tangu mwaka 2011. Mwaka huo, uchaguzi ulisitishwa mchana wakatiraia walikuwa wakipiga kura. Mwaka 2015, Uchaguzi Mkuu ulisogezwa mbele, kwa sababu ya tatizo la usalama. Na mwaka huu tena, zikisalia tu saa 5 kabla ya kuanza zoezi la kupiga kura, uchaguzi umeahirishwa, Yote haya yanachafua taifa hili, " amesema mtafiti huyo.

Wito wa kumuomba mwenyekiti wa INEC kuachia ngazi umeendelea kutolewa huku na kule nchini Nigeria.

Wapiga kura milioni 84 wanatarajia kupiga kura kumchagua rais mpya kati ya wagombea 72, ikiwa ni pamoja na rais anayemaliza muda wake Muhammadu Buhari.

Tume ya uchaguzi inasema ilifikia uamuzi wake baada ya kutafakari kwa kina kuhusu masuala ya usafirishaji wa vifaa na kufika kwa wakati kwenye vituo, changamoto ambayo tume hiyo ilisema isingewezekana kuwa na uchaguzi huru, haki na wakuaminika.

Hata hivyo mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, INEC, Mahmood Yakubu, akizungumza na wanahabari usiku wa kuamkia siku ya upigaji kura, alisema kwa ratiba ilivyo, isingewezekana tena kwa uchaguzi huo kufanyika kwa wakati.

Waangalizi wa kimataifa katika uchaguzi huo wametoa wito kwa raia wa taifa hilo kuwa watulivu wakati maandalizi ya uchaguzi yanaendelea.

Wagombea mbalimbali katika kiti cha urais ikiwa ni pamoja na rais anaye maliza muda wake Muhammadu Buhari na mpinzani wake Atiku Abubakar wameelezea kutoridhishwa kwao na hatua hiyo ya tume ya uchaguzi kusogeza mbele tarehe ya upigaji kura kwa madai ya kutokamilika kwa baadhi ya maandalizi muhimu.