DRC-SIASA

Wanasiasa DRC waomboleza kifo cha mwanasiasa kongwe Seneta Abdoulaye Yerodia

Abdoulaye Yerodia Ndombasi (picha ya kumbukumbu).
Abdoulaye Yerodia Ndombasi (picha ya kumbukumbu). © HENNY RAY ABRAMS / AFP

Jamii ya wanasiasa nchini DRC inaendelea kuomboleza kifo cha mwanasiasa kongwe seneta Abdoulaye Yerodia Ndombasi ambaye kifo chake kimetangzwa Jumanne asubuhi.

Matangazo ya kibiashara

Yerodia Ndombasi rafiki wa zamani wa karibu wa Kabila baba (Laurent Desire aliwahi kuwa mmoja wa makamu wa rais katika serikali ya mpito nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kati ya mwaka 2003 na 2006.

Abdoulaye Yerodia Ndombasi, rafiki wa zamani wa mwasisi wa mapinduzi nchini Argentina Ernesto Che Guevara, alizaliwa Januari 5, 1933, na alikuwa rafiki wa Waziri Mkuu wa China Zhou Enlai.

Yerodia Ndombasi alikuwa rafiki wa zamani wa Laurent Desire Kabila, baba wa Joseph Kabila, ambaye aling'oa utawala wa Marshal Mobutu Sese Seko. Abdoulaye Yerodia na Laurent Desire Kabila walikuwa na husiano wa karibu tangu enzi za vita vya uhuru mapema katika miaka ya 1960 kupitia mapambano makali kati ya mwaka 1964 na1965 katika vita vya maguguni vya Hewa Bora hadi kuchukuwa madaraka baada ya kuangusha utawala wa Mobotu Sese Seko mnamo mwezi Mei 1997.

Wakati huo Yerodia Ndombasi aliondoka Ufaransa na kurejea nyumbani DRC na kuteuliwa mkurugenzi katika ofisi ya rais Laurent-Desire Kabila kabla ya kuteuliwa waziri wa Mambo ya Nje.

Mnamo mwaka 1998, uasi ukichochewa na Rwanda ulizuka mashariki mwa DRC. Yerodia aliwataka wakazi wa eneo hilo kukabiliana na kuangamiza wavamizi. Wito ambao raia waliitikiwa kwa wingi hasa katika miji ya Kinshasa na Kisangani ambako watu walioshtumiwa uvamizi huo walichomwa wakiwa hai.

Kufuatia tukio hilo Ubelgiji ilitoa hati ya kimataifa ya kukamatwa Yerodia Ndombasi kwa uhalifu dhidi ya binadamu, ubaguzi wa rangi na mateso mengine.. Lakini waranti hiyo ilifutwa chini ya miaka miwili baadaye.

Kufuatia mikataba iliyofikiwa na makundi mbalimbali ya waasi, Abdoulaye Yerodia aliteuliwa Makamu wa rais wa Jamhuri kwa niaba ya serikali ya Kinshasa. Na mwaka 2006, alichaguliwa kama Senata.