NIGERIA-UCHAGUZI 2019

Wananchi wa Nigeria wanapiga kura kuchagua rais, milipuko yasikika

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari akipiga kura kwenye mji wa Daura. 23/02/2017
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari akipiga kura kwenye mji wa Daura. 23/02/2017 2019 presidential election in Nigeria Nigerian President Muhamma

Wananchi wa Nigeria wameanza kupiga kura kuchagua rais mpya baada ya uchaguzi huu kuahirishwa juma moja lililopita na kusababisha kuibuka kwa tuhuma za upangaji wa wizi wa kura hali iliyozidisha hofu kuwa yangetokea machafuko.

Matangazo ya kibiashara

Vituo zaidi ya laki 1 na elfu 20 vilifunguliwa maajira ya saa mbili kamili kwa saa za Nigeria na kushuhudia maelfu ya raia wakimiminika kwenda kwenye vituo hivyo kupiga kura.

Matokeo ya awali ya uchaguzi yanatarajiwa kuanza kutolewa kuanzia wiki ijayo ambapo mshindi ataongoza taifa hilo lenye utajiri wa mafuta kwa miaka minne ijayo.

Rais Muhammadu Buhari alikuwa miongoni mwa raia wa awali kabisa kupiga kura ambapo alifanya hivyo katika mji wa Daura, Kaskazini magharibi mwa jimbo la Katsina ambapo amesema anaamini atashinda uchaguzi huu.

“Mpaka sasa mambo mazuri, nitajipongeza mwenyewe, naenda kuwa mshindi”. Alisema rais Buhari wakati akiongea na waandishi wa habari baada ya kupiga kura.

Mpinzani wake wa karibu Atiku Abubakar mwenyewe alipiga kura kwenye jimbo lake la nyumbani la Adamawa, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Wapiga kura wanapaswa kuwachagua wawakilishi 360 watakaoingia katikabunge na maseneta 109 ambapo wagombea wa nafasi zote hizo wapo jumla ya elfu 65.

Hata hivyo saa chache kabla ya kuanza kwa zoezi la upigaji kura, kumeripotiwa mfululizo wa milipuko kaskazini mashariki mwa mji wa Maiduguri, mlipuko ambayo imeripotiwa kutekelezwa na wapiganaji wa kundi la kiislamu la Boko Haramu.

Nigeria: Roketi zilizoripotiwa kurushwa kwenye kambi ya wakimbizi walioko Maiduguri, Borno State. 23/2/2019.
Nigeria: Roketi zilizoripotiwa kurushwa kwenye kambi ya wakimbizi walioko Maiduguri, Borno State. 23/2/2019. RFIHAUSA/Bilyaminu Yusuf

Vyanzo vya usalama vimethibitisha pia kuripotiwa kwa mlipuko kwenye mji wa Auno ulioko umbali wa kilometa 25 na mji wa Geidam jirani na jimbo la Yobe.

Tume ya uchaguzi nchini humo INEC ilitangaza kuahirisha uchaguzi huu kwa juma moja kwa kile ilichodai kuwa wakati ule haikuwa tayari kuandaa uchaguzi ulio huru, haki na wakuaminika.

Uamuzi wa tume uliwakasirisha maelfu ya raia ambao walifanya safari ndefu kwenda kwenye maeneo yao kupiga kura na badala yake ukaahirishwa usiku wa kuamkia siku ya upigaji kura.

Zaidi ya wagombea 73 wanawania nafasi ya urais huku wapiga kura milioni 72 wakitarajiwa kupiga kura.