NIGERIA-UCHAGUZI-SIASA

Uchaguzi Nigeria: Muhammadu Buhari aendelea kuongoza, upinzani wadai wizi wa kura

Wananchi wa Nigeria walivyopiga kura Jumamosi Februari 23, 2019.
Wananchi wa Nigeria walivyopiga kura Jumamosi Februari 23, 2019. Luis Tato/AFP/Getty Images

Rais wa Nigeria Muhamadu Buhari ameendelea kuongoza katika matokeo zaidi ya kinganyairo cha urais, yanayoendelea kutangazwa na Tume ya Uchaguzi (INEC), huku chama kikuu cha upinzani PDP kikidai kutokea kwa wizi wa kura.

Matangazo ya kibiashara

Rais Buhari mwenye umri wa miaka 76, amemshinda mpinnzani wake Atiku Abubakar katika majimbo ya Kaskazini kama Niger, Jigawa na Kaduna, eneo ambalo lilionekana kuwa na ushindani mkali.

Hata hivyo, Atiku alimshinda Buhari katika jimbo la Abuja, makao makuu ya nchi huku ushindani mkali ukishuhudiwa katika majimbo la Kusini Mashariki na Magharibi mwa nchi hii.

Ili kupata ushindi, mgombea anastahili kupata asilimia 25 ya kura zote katika majimbo 24 kati ya 36 kote nchini ili kuzuia mzunguko wa pili.

Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa kwa namna matokeo haya yanavyokwenda, mshindi atapatikana katika mzunguko wa kwanza.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Mahmood Yakubu, amesema kila jitihada zinafanyika ili kumaliza zoezi la kutangaza matokeo hayo kutoka majimboni ili mshindi afahamike.

Chama kikuu cha upinzani PDP na kile cha APC, kinachotawala, vyote vimelaumiana kwa kudai kuwa, vinashirikiana na Tume ya uchaguzi kuiba kura.