SENEGAL-SIASA-UCHAGUZI

Senegal: Upinzani wafutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais

Idrissa Seck, wakati akisoma taarifa katika mkutano na waandishi wa habari baada ya kukutana na Khalifa Sall, Jumatatu, Januari 28, 2019.
Idrissa Seck, wakati akisoma taarifa katika mkutano na waandishi wa habari baada ya kukutana na Khalifa Sall, Jumatatu, Januari 28, 2019. © RFI/Guillaume Thibault

Wagombea wanne wa upinzani katika kiti cha urais nchini Senegal kupitia Waziri Mkuu wa zamani Idrissa Seck, wamefutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais yanayompa ushindi rais anayemaliza muda wake Macky Sall. Hata hivyo, wamebaini kwamba hawatofikisha malalamiko yao kwa Mahakama ya Katiba.

Matangazo ya kibiashara

Chini ya saa mmoja baada ya kutangazwa kwa matokeo ya awali ya uchaguzi, Idrisssa Seck katika mkutano na vyombo vya habari nyumbani kwake amesoma taarifa iliyowekwa pia saini na Ousmane Sonko, Issa Sall na Madicke Niang, wote wagombea katika kiti cha urais katika uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.

"Tume ya Taifa ya Kuhesabu Kura (CNRV) imetangaza matokeo yanayompa ushindi wa kishindo rais anayemaliza muda wake Macky Sall. Tunafutilia mbali matokeo hayo yamepangwa kwa kumpa ushindi usio halali Macky Sall.Kamwe hatutofikisha malalamiko yetu mbele ya Mahakama ya Katiba, "amesema Idrissa Seck ambaye amechukuwa nafasi ya pili kwa 20.50% ya kura, nyuma ya Macky Sall ambaye amepata 58.27%, kulingana na matokeo ya awali ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Kuhesabu Kura (CNRV).

Wengi walitarajia kuwa kutakuepo na duru ya pili ya uchaguzi, wakibaini kwamba katika ya wagombea wote watano hakuna atakayetimiza asilimia 50 ya kura.

Upinzani umeishushia lawama Tume ya Uchaguzi (CENA) kwamba iliandaa uchaguzi kwa njama za kumpa ushindi Macky Sall.

Madai ambayo Tume ya Uchaguzi na kambi ya Macky Sall wamekanusha.