COMORO-SIASA-USALAMA

Watu watatu wenye silaha wauawa Comoro

Moroni, mji mkuu wa visiwa vya Comoro.
Moroni, mji mkuu wa visiwa vya Comoro. TONY KARUMBA / AFP

Vikosi vya usalama vya Comoro vimeua watu watatu wenye silaha wakati wa urushianaji risasi karibu na kambi ya jeshi ya mji mkuu Moroni, kufuatia kutoroka kwa askari waasi gerezani.

Matangazo ya kibiashara

Mapigano kati ya watu wenye silaha na vikosi vya usalama yalidumu saa moja. Waziri wa Mambo ya Ndani Mohamed Daoudou amebaini kwamba kundi la askari walioasi, ambao walikuwa wanazuiliwa jela kwa jaribio la mapinduzi la mwaka jana, walitoroka Alhamisi asubuhi na kwenda katika kambi ya jeshi kwa matumaini ya kuwashawishi askari kuwaunga mkono.

Kiongozi wao, Fayssoil Abdoussalam, aliyekuwa na cheo cha kamanda, ni miongoni mwa watu hao watatu waliouawa, amesema Waziri wa Mambo ya Ndani. Awali vyanzo vya kijeshi na vyombo vya usalama vilikuwa vimesma kuwa watu wanne waliouawa katika urushianaji risasi.

"Fayssoil alijaribu kuwashawishi baadhi ya askari kwa lengo lake hilo lakini hawakumfuata," Mohamed Daoudou amewaambia waandishi wa habari, akiongeza kuwa hali ya utulivu imerejea.

Azali Assoumani alitangazwa kuwa mshindi wa kiti cha rais baada ya uchaguzi wa Jumapili kwa 60% ya kura. Ujumbe wa waangalizi wa Afrika, ikiwa ni pamoja na ule wa Umoja wa Afrika (AU), ulihitimisha kuwa uchaguzi haukuwa wa kuaminika na wa wazi.

Saa chache kabla ya tukio hilo la Alhamisi, Washindani 12 wa Azali Assoumani katika kinyang'anyiro cha urais walisema wataunda taasisi ambayo lengo lake litakuwa la kumwondoa madarakani. Baraza lao la Taifa la Mpito litaongozwa na mmoja wao, Mkuu wa zamani majeshi Mohamed Soilihi."

Kazi ya Baraza la Taifa la Mpito ni kutatua mgogoro wa baada ya uchaguzi, kuhakikisha mabadiliko kwa njia ya amani, kutunza amani, utulivu na msikamano wa kitaifa katika nchi yetu," alisema Soilihi katika tangazo lililorushwa kwenye vituo vya redio nchini Comoro na mitandao ya kijamii.

Vyanzo vya kidiplomasia vinasema kuwa Soilihi alikamatwa baada ya kutoa tangazo hilo. Mamlaka imeamuru kufungwa kwa gazeti la La Gazette, kwa sababu lilichapisha makala juu ya Baraza la Mpito la Taifa.