BURKINA FASO-USALAMA-MAUAJI

Sitini na mbili wauawa Arbinda, Burkina Faso

Jumapili usiku, watu wenye silaha walivamia kijiji cha Hamkan, kilomita 7 kutoka Arbinda, ambapo waliua kiongozi wa kidini wa kijiji hicho na watu kutoka familia yake.
Jumapili usiku, watu wenye silaha walivamia kijiji cha Hamkan, kilomita 7 kutoka Arbinda, ambapo waliua kiongozi wa kidini wa kijiji hicho na watu kutoka familia yake. © Google Maps

Watu wasiopungua sitini na mbili waliuawa wiki iliyopita katika machafuko ya kikabila nchini Burkina Faso, kwa mujibu wa mamlaka nchini humo. Viongiozi mbalimbali wametembelea eneo la tukio.

Matangazo ya kibiashara

Machafuko hayo yalianza usiku wa Machi 31, karibu na mji wa Arbinda, katika Jimbo la Soum, wakati kiongozi wa kidini na watu sita kutoka familia yake waliuawa na wapiganaji wasiojulikana, Chama tawala cha MPP kimesema, katika taarifa yake.

"Asubuhi ya Aprili 1, kulishuhudiwa vitendo vya ulipizaji kisasi katika Wilaya ya Arbinda, ambavyo viliendeshwa dhidi ya jamii moja baada ya kuuawa kwa kiongozi wa kidini," taarifa hiyo imesema.

Waziri wa Nchi, Simeon Sawadogo, amesema kwenye televisheni ya serikali kwamba watu 62 waliuawa katika shambulio hilo huko Arbinda.

"Watu thelathini waliuawa katika machafuko ya kikabila, na wengine 32 waliuawa na magaidi," amesema.

Katika Jimbo jirani la Bulgou, watu kutoka familia ya kifalme ya kijadi ya Zoaga pia walishambuliwa na watu tisa waliuawa, kwa mujibu wa ripoti ya awali.