SUDANI-SIASA-USALAMA-MAANDAMANO

Vyanzo kadhaa: Rais Omar al Bashir amejiuzulu

Magari ya kijeshi ya Sudan yametumwa Alhamisi asubuhi kwenye madaraja ya Mto Nile na katika maeneo muhimu ya mji mkuu, Khartoum, ambapo watu wameonekana wakiimba "amenguka, tumeshinda!" wakimaanisha rais Omar al-Bashir, mwandishi wa shirika la Habari la Reuters ameripoti.

Waandamanaji wakisabahi askari jijini Khartoum, Aprili 10, 2019.
Waandamanaji wakisabahi askari jijini Khartoum, Aprili 10, 2019. TWITTER/@THAWRAGYSD/via REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Vyanzo kadhaa vimebaini kwamba rais Omar al-Bashir amejuzulu, na manzungumzo yameanza ili kuunda serikali ya mpito.

Omar al-Bashir na maafisa kadhaa katika serikali yake wako chini ya ulinzi mkali, kwa mujibu wa vyanzo hivyo.

Lakini kiongozi wa upinzani, Omar Saleh Sennar, ameliambia shirika la Habari la Reuters kwamba waandamanaji dhidi ya utawala wa Bashir utakubalii tu serikali ya kiraia inayojumuisha wanasiasa wa upinzani.

"Tutakubali tu serikali ya mpito ya kiraia inayojumuisha wadau wote katika kutetea Uhuru na mabadiliko," amesema Saleh Sennar.

Maelfu ya watu wameungana na wenzao wanaokusanyika mbele ya makao makuu ya jeshi tangu mwanzoni mwa wiki hii, kwa mujibu wa shirika la Habari la Reuters.

Mapema asubuhi, televisheni ya taifa imeripoti kuwa jeshi linajiandaa kutoa tangazo muhimu. Matangazo ya redio yamekatizwa, badala yake kumewekwa muziki wa kijeshi.

Raia nchini Sudan wanasubiri kwa hamu kile ambacho vyombo vya hanari vya kitaifa vinaeleza kuwa ni tangazo muhimu kutoka kwa jeshi.

Kumeshuhudiwa maandamano ya miezi kadhaa ya umma ya kumshinikiza rais al-Bashir ajiuzulu.

Rais Omar al-Bashir ambaye yuko madarakani tangu mwaka 1989 anakabiliwa na maandamano tangu mwezi Desemba mwaka jana ya kumtaka ajiuzulu.