LIBYA-UFARANSA-EU-USALAMA

Ufaransa yazuia tangazo la Umoja wa Ulaya linalomshtumu Haftar

Ufaransa imepinga kuchapishwa kwa tangazo la Umoja wa Ulaya linalomtaka Marshal Khalifa Haftar, ambaye majeshi yake yanadhibiti eneo la mashariki mwa Libya, kusitisha mapigano aliyoanzisha kwa minajili ya kuteka mji mkuu Tripoli, vyanzo vya kidiplomasia vimesema.

Magari ya kijeshi ya vikosi vy Misrata, chini ya ulinzi wa majeshi ya Tripoli, yameonekana katika eneo jirani la Tajura, mashariki mwa Tripoli, Libya, Aprili 6, 2019.
Magari ya kijeshi ya vikosi vy Misrata, chini ya ulinzi wa majeshi ya Tripoli, yameonekana katika eneo jirani la Tajura, mashariki mwa Tripoli, Libya, Aprili 6, 2019. REUTERS/Hani Amara
Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa Shirika la habari la Reuters, rasimu hiyo ya tangazo, inabaini kwamba mashambulizi ya kijeshi yaliyozinduliwa na majeshi ya Marshal Khalifa Haftar (ANL) dhidi ya mji mkuu Tripoli " yanatishia usalama wa raia, yanahatarisha mchakato wa kisiasa na yanaweza kuzua mvutano na matokeo makubwa mabaya kwa Libya na kanda nzima kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na tishio la kigaidi ".

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mapigano kati ya majeshi ya ANL na vikosi vya serikali inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa (GNA) yamesababisha maelfu ya waakazi wa viunga vya mji mkuu Tripoli kutoroka makaazi yao.

Kutoafikiana kwa rasimu hii ya tangazo inaonyesha tofauti kati ya wanachama wa Umoja wa Ulaya kuhusu suala la Libya.

Jumatano wiki hii rais wa Bunge la Ulaya alilaumu mgawanyiko huo kati ya Ufaransa na Italia licha ya msimamo mmoja ulioonyeshwa na diplomasia ya Ulaya.

Rais wa Bunge la Ulaya, Antonio Tajani, raia wa Italia, alizitaka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuzungumza kwa kauli moja dhidi ya kuongezeka kwa machafuko nchini Libya.

Hata hivyo Ufaransa ilipinga rasimu hiyo ya tangazo iliyoandikwa Brussels, kupitia mchakato ambao unaruhusu kila nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya kupinga mapigano hayo.

Ujumbe wa kidiplomasia wa Ufaransa mpaka sasa haujatoa tamko lolote kuhusiana na madai hayo, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.