LIBYA-UN-UFARANSA-USHIRIKIANO

Serikali ya Tripoli yashutumu jumuiya ya kimataifa na Ufaransa

Majeshi ya serikali ya Libya, Ain Zara, Tripoli, Libya, Aprili 25, 2019.
Majeshi ya serikali ya Libya, Ain Zara, Tripoli, Libya, Aprili 25, 2019. © REUTERS/Hani Amara

Wakati mapigano yanaendelea kurindima kusini mwa mji mkuu wa Libya, serikali ya Tripoli imeanzisha vita vya kidiplomasia. Licha ya uungwaji mkono wa Umoja wa Mataifa, serikali ya Tripoli imeshtumu msimamo wa jumuiya ya kimataifa na hasa msimamo wa Ufaransa.

Matangazo ya kibiashara

Mnamo Aprili 18, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tripoli, Fathi Bachagha, aliamua kusitisha ushirikiano wa mafunzo ya kiusalama na Ufaransa, akishtumu nchi hiyo kumsaidia Khalifa Haftar. Waziri alisisitiza juu ya uhuru wa nchi yake kwa kutetea hatua zake na kauli yake.

"Kwa hali ya sasa, kutokana na msaada wa Ufaransa kwa Haftar na serikali yake, ninavichukulia sawa na Vita Kuu ya II wakati Ujerumani iliposaidia serikali ya isiyo halali ya Vichy", amesema Waziri fathi Bachagha.

Hata hivyo waziri Bachagha amenyooshea kidole mgawanyiko wa kimataifa unaodhoofisha kazi ya Umoja wa Mataifa. Kwa mjubu wa Waziri Bachagha, Libya inaathirika kufuatia diplomasia inayokuwa kwa bidhaa ya petroli, hasa kutoka Falme za Kiarabu.

"Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya unataka kusaidia nchi hii," amesema waziri, "lakini tunaona kuwa maslahi ya fedha na rushwa ya kisiasa vina nguvu zaidi kuliko nia ya Umoja wa Mataifa."

Bachagha anaona kuwa uchaguzi, mazungumzo, mikataba ya kisiasa vinaweza kuleta suluhu, lakini aamekataa uwepo wa Khalifa Haftar kwa yote hayo.