DUNIA-UISLAMU-HAKI

Mamilioni ya Waislamu waanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan

Mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan waanza kwa Waislamu. Mwezi wa Ramadhan ni mwezi wa kusoma sana Q'uran.
Mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan waanza kwa Waislamu. Mwezi wa Ramadhan ni mwezi wa kusoma sana Q'uran. © SIMON MAINA / AFP

Mamilioni ya Waislamu duniani kote leo wameanza kufunga kwa ajili ya mwezi mtukufu wa Ramadhan ambapo hujizuwiya kula na kunywa kuanzia aljajiri hadi jua linapozama takriban siku 30 au 29 kutegemea na muandamo wa mwezi.

Matangazo ya kibiashara

Ramadhan huanza mwezi wa tisa wa kalenda ya Kiislam ambapo Waislam wanaamini Kuran takatifu iliwasilishwa kwa Mtume Mohammad katika karne ya saba mnamo mwezi wa Ramadhan.

Waislamu wanaamini kuwa huu ni mwezi wa kupatiwa msamaha na Mwenyenzimungu kwa hiyo huzidisha ibada kwa wingi na kuwa karibu na Mwenyeenzi-Mungu.

Saudi Arabia mahala kulikozaliwa Uislamu pamoja na nchi kadhaa za Mashariki ya Kati,Ghuba na nchi nyingi za Kiislam ikiwemo Indonesia taifa lenye idadi kubwa kabisa ya Waislamu duniani na Ulaya Waislamu wameanza kufunga leo Jumatatu kutimiza nguzo ya tano ya Uislamu, mwezi ambao aya ya kwanza ya Q'uran iliteremshwa kwa Mtume Muhammad (SAW).

Ni wakati ambapo Waislamu hutafakari kwa undani kabisa matendo yao, kuwa wanyenyekevu zaidi kwa Mwenyeenzi-Mungu kwa kufuata maamrisho yake na kuachana na maovu yote alilyoyakataza pamoja na kuweza kujizuwiya na matamanio.

Kwa mujibu wa Sheikh Haruna Kigabiro, “mwezi wa Ramadhan ni mwezi uliojaa rehema na fadhila”.

“Ramadhan kwa Waislamu ni mwezi wa aina yake ni mwezi wa kumcha Mungu na hukamilishwa baada ya mwezi mmoja kwa sherehe za Idd el Fitr.” ameongeza Sheikh Kigabiro.

Waislamu wanasema huu ni mwezi wa toba wa kuomba msamaha kwa Mwenyeenzi-Mungu ili kufutiwa madhambi.

Nchini Marekani inakadiriwa Waislam zaid ya milioni 3 watafunga mnamo mwezi huu wa Ramadhan ikiwa ni karibu asilimia 10 ya wakaazi milioni 327 wa nchi hiyo.